Kibaha yaomba Sh4 bil kujenga hospitali ya wilaya

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha,Tatu Selemani

Muktasari:

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Tatu Selemani alisema hayo jana kwenye kikao cha bajeti kilichohudhuriwa pia na watendaji na viongozi wa vyama vya siasa.

 Wahenga walisema, ukienda kuomba mboga kwa jirani nenda na yako iliyochacha. Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imetenga Sh121 milioni na kisha kuwasilisha maombi maalumu serikalini ya kupatiwa Sh4.2 bilioni ili kujenga hospitali ya wilaya katika eneo la Mlandizi kutokana na kituo cha afya kilichopo kuzidiwa na wagonjwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Tatu Selemani alisema hayo jana kwenye kikao cha bajeti kilichohudhuriwa pia na watendaji na viongozi wa vyama vya siasa. Alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na changamoto wanazopata katika utoaji huduma kwenye Kituo cha Afya Mlandizi hasa mrundikano mkubwa wa wagonjwa kutokana na kutumika kama hospitali ya wilaya huku kituo hicho kikihudumia pia maeneo jirani kama Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mjini.

Akichangia hoja hiyo, diwani viti maalumu, Josephine Gunda alisetaka katika bajeti ya 2018/19 halmashauri pia itenge Sh70 milioni kwa ajili ya zahanati za Madege, Kigola, Mpiji makazi mapya, Madimla, Vikuruti na Kisabi kwani bado wananchi wa maeneo hayo wanakosa huduma za afya na kulazimika kuzifuata Mlandizi.

Diwani wa Boko Mnemela, Mohamed Samata alishauri bajeti ya mwaka huu iendane na maboresho katika ofisi za watendaji wa kata kama ilivyo kwa idara zingine.

Hata hivyo, mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa alitaka vikao vya bajeti viwe vinafuata kalenda kwani wakati huu tayari mapendekezo ya bajeti inayojadiliwa ilishafika ngazi ya mkoa.

Awali, ofisa mipango wa wilaya hiyo, Matha Mbijili aliwasilisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka 2018/2019 akisema Sh32.9 bilioni zitakusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali.