Kibaha yatekeleza agizo la Magufuli kuhusu malaria

Muktasari:

  • Rais Magufuli aliagiza halmashauri nchini kutumia sehemu ya mapato yake kupambana na malaria

 Mazalia 261 ya mbu waenezao malaria yamegundulika na kunyunyiziwa dawa mjini Kibaha mkoani Pwani.

Mratibu wa Malaria mjini Kibaha, Ali Shaha alisema mazalia hayo yamegundulika kwenye kata tano kati ya 12 katika awamu ya kwanza ya unyunyiziaji huo, lakini lengo ni kuendesha operesheni nchi nzima.

Shaha alitoa takwimu hizo kwenye tamasha la malaria lenye kaulimbiu ‘Zama zimebadilika siyo kila homa ni malaria nenda kapime’, linaloendeshwa mkoani Pwani na shirika linalojihusisha na masuala ya afya la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC).

“Kibaha maambukizi ya malaria yameshuka maana mwaka 2016 mjini ugonjwa huo ulikuwa ni asilimia 13 lakini mwaka 2017, tumefanya utafiti tukabaini imeshuka mpaka 10,” alisema Shaha na kuongeza: “Kata tulizonyunyizia ni Tangini, Tumbi, Mkuza, Pichandege na Mailimoja.”

Dawa ya viuadudu iliyotumika ni kati ya lita 520 zenye thamani ya Sh6.7 milioni, zilizopokelewa na halmashauri Juni kutoka Kiwanda cha Biotech Product ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kila wilaya kutumia mapato yake kuulia mbu waenezao malaria.

Awali, Meneja wa TCDC, Antony Nacasenga alisema kampeni ya zama zimebadilika inafanywa na shirika hilo chini ya Wizara ya Afya katika mikoa ya Lindi, Pwani, Kagera, Mtwara na Ruvuma na wamelenga kufikia wilaya 34 Tanzania Bara.

Nacasenga alibainisha kuwa wanalenga maeneo manne; moja kuhamasisha wananchi kwenda kupima katika zahanati au vituo vya afya kabla ya kutumia dawa kutokana na dhana iliyojengeka mtu akihisi homa anajua ni malaria.

Pia, alisema wanatoa elimu kwa wanaokwenda kupima na kupewa ushauri na wataalamu ili wazingatie ratiba za umezaji dawa kama wanavyoelekezwa na kukamilisha dozi. Alisema utafiti unaonyesha wengi humeza nusu na wakijisikia nafuu hukatisha dozi, wakijua wamepona hivyo kuifanya malaria kuwa sugu.