Kichaa cha mbwa huua watu 1,500 kila mwaka nchini

Muktasari:

  • Magonjwa yatokanayo na kichaa cha mbwa yamekuwa yakiligharimu Taifa fedha nyingi

Dodoma. Wakati watu 60,000 hufariki dunia kila mwaka ulimwenguni kutokana na kung’atwa na mbwa, kwa hapa nchini watu 1,500 hufa huku wengi wao wakiwa watoto kutoka vijijini.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kitengo cha wanyama ilieleza kuwa mabara ya Afrika na Asia yanaongoza kwa vifo hivyo.

Inaeleza kuwa magonjwa yatokanayo na kichaa cha mbwa yamekuwa yakiligharimu Taifa fedha nyingi katika matibabu ya watu wanaong’atwa na mbwa.

Mkurugenzi msaidizi wa huduma za wanyama, Dk Martin Ruheta alisema idara ya wanyama katika Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Chakula Duniani (FAO) na mashirika mengine, wameandaa mkakati wa kuzuia vifo vitokanavyo na mbwa ifikapo mwaka 2030.

Dk Ruhata alisema mpango huo unashirikisha mashirika ya kimataifa, taasisi za ndani na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani ili kutoa elimu kwa jamii katika kuitumia Septemba 28 kama siku ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mapambano ya kutokomeza vifo vitokanavyo na mbwa.

“Mpango huo unajulikana kama O by 2030 ambao unalenga kuanzisha mapambano hayo ili kufikiwa malengo tunayotarajia, taasisi kama za Ifakara Health Institute, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Taasisi ya Mandela na wenzetu wengine kutoka nje katika vyuo vya Washington na Glasgow ambao pia watashiriki katika siku hiyo muhimu kwetu,” alisema Dk Ruheta.

Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wagonjwa 28,000 waling’atwa na mbwa mwaka 2017 pekee.