Kifo cha Akwilina ni mfano wa nyota iliyozimika ghafla

Muktasari:

  • Ni siku ambayo angeianza ndoto yake kwa kuonyesha uwezo wake katika kile alichojifunza katika mwaka wake wa kwanza wa masomo ya shahada ya ununuzi na ugavi aliyoyapata chuoni hapo.

Jumatatu ya Februari 26 ni siku ambayo mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwiline alikuwa aanze mafunzo ya vitendo mjini Bagamoyo.

Ni siku ambayo angeianza ndoto yake kwa kuonyesha uwezo wake katika kile alichojifunza katika mwaka wake wa kwanza wa masomo ya shahada ya ununuzi na ugavi aliyoyapata chuoni hapo.

Hata hivyo katika hali ya kusikitisha Ijumaa ya Februari 16, uhai wake ulikatishwa ghafla.

Ndoto yake ya kuonyesha kwa vitendo kile alichojifunza NIT na pengine kuweka mazingira ya kupata ajira vyote vilizimika katika mazingira yaliyowaachia simanzi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa ujumla.

Ilikuwa mfano wa mshumaa au nyota iliyozimika ghafla wakati kila mmoja akiwa na matarajio makubwa ya kupata nuru.

Siku ya tukio Akwilina alikuwa kwenye basi akielekea Kituo cha Makumbusho ili apande basi jingine la kwenda Bagamoyo kupeleka barua ambayo ingempa nafasi ya kuanza mafunzo kwa vitendo.

Akwilina alipigwa risasi katika vurugu zilizohusisha polisi waliokuwa wakipambana na wafuasi wa Chadema walioandamana kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kudai barua za mawakala wa kusimamia uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Kabla ya kifo cha Akwilina, siku hiyo hiyo vyama vitatu vikubwa vilikuwa na mikutano ya kufunga kampeni.

CCM walikuwa wakifunga kampeni Uwanja wa Biafra, Chadema walikuwa Uwanja wa Buibui na CUF walikuwa Mwananyamala kwa Mama Zakaria.

Katika mkutano wa Chadema, mwenyekiti wao, Freeman Mbowe alimlalamikia msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aaron Kagulumjuli kwa kuwanyima barua za viapo za mawakala wa chama hicho.

INAENDELEA UK28

INATOKA UK 27

Jana yake (Februari 15), Mbowe aliwaongoza baadhi ya viongozi wa chama hicho kwenda makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kudai barua hizo na waliambiwa zinashughulikiwa.

Hadi Februari 16 jioni walikuwa hawajapewa barua hizo ndipo Mbowe akiwa katika mkutano wa kampeni baada ya mgombea wa chama hicho, Salum Mwalimu kuhutubia, aliamuru wanachama na viongozi waliokuwa hapo kuzifuata barua hizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

Maandamano yalianzia Mwananyamala Komakoma kuelekea Kinondoni Studio kisha kituo cha Mkwajuni ambapo ndipo walipokutana na upinzani wa polisi.

Katika mapambano hayo ndipo mwanafunzi huyo alipouwawa na tayari taarifa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inaonyesha aliuliwa kwa kupigwa risasi.

Mashuhuda

Kondakta wa basi alilopanda Akwilina kwenda makumbusho, Abbas Abdallah anasema baada ya abiria kupungua, Akwilina aliamua kwenda kukaa siti ya nyuma iliyokuwa wazi lakini ghafla wakaanza kusikia kelele za abiria ndani ya basi.

Abdallah alijeruhiwa usoni wakati huo Akwilina alikuwa chini anatokwa damu huku kelele za abiria zikiendelea na ndipo dereva alipomwambia Abdallah alale chini.

Akielezea zaidi dereva wa gari hilo, Shaaban Mohamed anasema aliamua kuendesha gari hadi Kituo cha Studio Kinondoni na kumwambia trafiki aliyekuwa eneo kuhusu abiria aliyeumia.

Trafiki huyo aliwaelekeza wampeleke polisi ambako walipewa askari waliyekwenda naye Mwananyamala Hospitali.

Akiwa hapo ndipo alipogundua kwamba abiria huyo aliyeanguka chini (Akwilina) alikuwa ameshafariki dunia na huo ukawa mwisho wa ndoto za Akwilina. Baadaye mwili wa Akwilina ulihamishiwa Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akizungumzia zaidi tukio hilo, dereva huyo anasema kwamba mbali na kifo hicho pamoja na kondakta kujeruhiwa, gari lao pia lilivunjika baadhi ya vioo.

Ndugu walivyopokea msiba

Akwilina ambaye kwao ni kijiji cha Olele, Rombo mkoani Kilimanjaro alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya elimu huku ndugu zake wakiwa na matumaini makubwa kwake kama anavyolalamika dada wa Akwilina aitwaye, Tugoleana Uiso.

“Sitakuona tena mdogo wangu, ulikwenda kusoma na mkopo ulipata asilimia 100, wazazi nyumbani walikuwa wakikutegemea ungewasaidia.”

“Nilikwambia mdogo wangu soma kwa bidi ili uje utuokoe, bahati nzuri mkopo ukapata kwa asilimia 100, sasa mbona hujatimiza ahadi yako, mbona umekufa ghafla?”

Tugoleana alibainisha kwamba Akwilina ni mtoto pekee katika familia yao aliyefikia elimu ya juu na asingepata mkopo kwa asilimia 100 asingeweza kuendelea na masomo.

Hali hiyo ya majonzi pia walikuwa nayo ndugu wengine, majirani, jamaa na marafiki hasa wanafunzi wenzake ambao waliokuwa Mbezi Louis kwenye msiba.

Akwiline Shirima ambaye ni baba wa Akwilina naye alielezea uchungu na hasira alizokuwa nazo kwa muuaji wa mtoto wake huku akielezea namna alivyokuwa na matumaini na mwanaye huyo na kuiomba Serikali kuangalia namna ya kumsaidia.

“Jamani hii ni taa yangu, imezimika na kuniacha gizani kwani tangu nimepata taarifa sijaweza kula chochote, nimekuwa mfano wa nguruwe aliyetelekezwa porini,’’ alisema.

Rafiki wa Akwilina, Hidaya Shaaban akizungumzia tukio hilo anasema, “Akwilina aliniaga anaenda Bagamoyo kupeleka barua ya kuomba field (mafunzo kwa vitendo) lakini jioni nikashituka kusikia amepata ajali, baadaye nikaambiwa amekufa.”

Awali familia ya Akwilina ilikataa kuupokea mwili wa mtoto wao kwa madai kwamba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili haikuwapa ripoti ya uchunguzi wa kilichosababisha kifo kwa madai kwamba ripoti hiyo ingetolewa baada ya siku 14.

Hata hivyo baadaye ripoti hiyo ilitolewa na kuonyesha kuwa Akwilina alifariki baada ya kichwa chake kupasuliwa kwa risasi ambayo iliingia upande wa kushoto na kutokea upande wa kulia.

Serikali ilivyoupokea msiba

Wakati Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini akiomba iundwe tume huru kuchunguza mauaji hayo. Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.

Mbali na waziri huyo, Rais John Magufuli naye mbali na kuelezea kusikitishwa na kifo hicho pia amelitaka jeshi hilo kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na mauaji hayo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliitembelea familia ya marehemu Mbezi Luis na kuahidi kugharamia msiba huo, huku pia akitaka uchunguzi wa vyombo vya dola ufanywe haraka.

Mbali na Waziri Ndalichako, naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni naye alisisitiza mpango wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alikiri kutokea mauaji hayo ya risasi alipozungumza kwa njia ya simu na gazeti hili.

Februari 19 kamanda huyo alisema kwamba jeshi hilo linawashikilia askari wake sita na watuhumiwa 40 kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.

Tayari jeshi hilo limeshawaita viongozi wa Chadema akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji kuripoti katika kituo kikuu cha Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Wengine ni wabunge Esther Matiko, John Heche, John Mnyika na Halima Mdee pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya chama hicho, Salum Mwalimu.

Mwili wa Akwilina unatarajiwa kuagwa kesho kwenye viwanja vya NIT kabla ya mazishi ambayo yanatarajia kufanyika keshokutwa huko Rombo na hivyo kuhitimisha safari ya msomi huyo ambaye anabaki kuwa mfano wa nyota iliyozimika ghafla.