Kigogo KCBL ahojiwa dawa za kulevya

Muktasari:

Habari za uhakika zinadai Hosea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), alikamatwa Alhamisi iliyopita na kuhojiwa kabla ya nyumba yake kupekuliwa.

Mfanyabiashara wa Moshi, Reginald Hosea anachunguzwa na Polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Habari za uhakika zinadai Hosea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), alikamatwa Alhamisi iliyopita na kuhojiwa kabla ya nyumba yake kupekuliwa.

Hata hivyo, Hosea mwenyewe alipohojiwa kuhusiana na tuhuma hizo, alithibitisha kukamatwa na kuhojiwa na polisi kisha kuachiwa kwa dhamana lakini akakanusha kujihusisha na biashara hiyo.

“Kwa sasa bado ni mapema mno kuzungumzia jambo hilo kwa sababu hata sijui ni nani hasa alipeleka taarifa hizo polisi na kwa malengo gani. Tuache polisi waendelee na uchunguzi wao,” alisema Hosea.

Hosea ambaye pia ni mjumbe wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alisema katika maisha yake hajawahi kuuza hata pombe.

Habari zinadai mfanyabiashara huyo alikamatwa na polisi ambao walimchukua hadi nyumbani kwake eneo la Soweto mjini Moshi, kisha kupekua nyumba yake kwa saa kadhaa lakini hawakupata dawa hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alipoulizwa jana kuhusu suala hilo alisema alikuwa hajapelekewa taarifa hiyo, lakini akaahidi kufuatilia kwa sababu linaweza kuwa linashughulikiwa na askari wake wa chini.

Vita ya dawa za kulevya

Akihutubia wakazi wa jijini Arusha juzi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid baada ya kutunuku kamisheni kwa maofisa 422 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Rais John Magufuli alisema vita ya kupambana na dawa za kulevya haitasimama hadi ushindi upatikane.

Rais Magufuli alisema wakati Serikali yake inaingia madarakani kulikuwa kuna mtu anatafutwa nchi za nje kwa tuhuma za kuwa kinara wa dawa za kulevya, tayari amekamatwa na kusafirishwa nchini Marekani.

Alisema tayari mtuhumiwa huyo aliyemtaja kuwa anaitwa Shkuba, tayari amepelekwa Marekani na akiponyoka huko, akirudishwa nchini watahangaika naye.

“Vijana wakishavuta dawa za kulevya wanatoka makamasi kutwa nzima, huyu hawezi kwenda kufanya kazi wakati tunasimamia tunakazania kufanya kazi, lazima wahusika wakamatawe,” alisema.