Kigogo Temesa asimamishwa, kamati ya uchunguzi yaundwa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Tamesa, Dk Mussa Mgwatu na kuunda kamati ya watu saba kuchunguza tukio la kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Dk Mussa Mgwatu ili kupisha uchunguzi wa tukio la kuzama Kivuko ya Mv Nyerere.

Pia, Majaliwa ameunda kamati ya watu saba kuchunguza tukio hilo itakayoongozwa na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara ambayo itafanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Akizungumza leo Septemba 24, 2018 katika eneo la Ukara, wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Majaliwa amesema kwa mamlaka aliyopewa, baada ya Rais John Magufuli kuivunja bodi ya Temesa, Dk Mgwatu atakaa kando hadi uchunguzi utakapokamilika ili  kubaini uzembe uliosababisha tukio hilo.

Majaliwa amewataja wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi, Mhandisi Maselina Magesa aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Temesa.

Wengine ni Wakili Julius Kalolo ambaye atasaidia mapitio ya sheria na mfumo mzima wa uendeshaji vivuko, Queen Mlozi atakayesimamia stahiki za kina mama na Camilius Wambura na Bashiru Hussein kutoka ofisi ya Waziri mkuu upande wa maafa.

“Kazi hii ianze mara moja na ninataka ndani ya mwezi mmoja wawe wamekamilisha uchunguzi wao, naamini majeshi huwa hatuna vikao vingi, ikamilike mapema,” amesema Majaliwa.