Kigogo wilaya kortini kwa kumtusi DC

Muktasari:

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Naomi Mwerinde, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bernad Machibya alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 17, mwaka huu.

Rombo. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Evarist Silayo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Rombo akikabiliwa na kosa la kumtolea lugha ya matusi Mkuu wa wilaya hiyo, Agnes Hokororo.

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Naomi Mwerinde, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bernad Machibya alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 17, mwaka huu.

Alidai kuwa Silayo alitenda kosa hilo katika eneo la Rombo Mkuu kwa kumwambia mkuu huyo wa wilaya kuwa, “acha siasa za kipuuzi, huo ni upumbavu ukiendelea utaondoka kama mwenzio Kipuyo.”

Mshtakiwa huyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngoyoni wilayani hapa, alikana shtaka hilo na mwendesha mashtaka wa polisi alidai kwamba upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao walisaini hati ya Sh1 milioni. Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Septemba 26.

Wakati huohuo, Ebenezer Heromini Woisso (16), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Olele amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa la kumbaka na kumtia mimba mdogo wake mwenye umri wa miaka 14.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Machibya alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo mwaka huu katika Kijiji cha Kooti - Mashati, kwa kumbaka mdogo wake wa kuzaliwa naye tumbo moja.

Machibya alidai mshtakiwa alimbaka mdogo wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Horombo wilayani humo.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.