Kigoma, Kagera vinara kuzaa watoto wengi

Muktasari:

Imeelezwa kuwa kwa wastani mwanamke wa Kitanzania anazaa watoto 5.2.

Dar es Salaam. Utafiti mpya umeonyesha kuwa wanawake wanaotoka mikoa ya kusini wanazaa watoto wachache zaidi ukilinganisha na wale wa mikoa ya Kigoma na Kagera.

Imeelezwa kuwa kwa wastani mwanamke wa Kitanzania anazaa watoto 5.2.

Hayo yameelezwa katika uzinduzi wa ripoti ya matokeo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2015/2016.

Utafiti huo unaonyesha wanawake kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na Arusha wanazaa kwa wastani wa 3.8 mpaka 4.2, huku mikoa inayoongoza kwa kupata watoto wengi ni Kigoma na Kagera ambayo wao huzaa wastani wa watoto 6.8.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliwataka wanawake wazingatie uzazi wa mpango kwa kuzaa watoto watakaoweza kuwatunza na kuwapa huduma zote muhimu.

Alisema umefika wakati kwa wanawake kupunguze kuzaa watoto bila malengo ili kuepuka wimbi la watoto wa mitaani.

“Wanawake na wasichana tumieni njia za uzazi wa mpango kwa kuzaa watoto mnaoweza kuwatunza ili kujenga Tanzania ya viwanda kwani kwa wastani wa ongezeko la idadi ya watu nchi yetu inaongoza, bado juhudi zinahitajika kwa wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya uzazi wa mpango,” alisema Waziri Ummy.

Utafiti huo ulibaini kuwa uwiano wa mimba za utotoni umekua kutoka wastani wa asilimia 23 mwaka 2010 mpaka kufikia asilimia 27 mwaka jana.

Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa alisema katika kutekeleza malengo 17 ya milenia yenye shabaha 169 na viashiria 230, yote yanahitaji watu wenye afya njema ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kutimiza azma iliyowekwa na dunia ifikapo mwaka 2030.

Alisema takwimu za utafiti huo ni rasmi na zinatumika katika kuboresha Sera za Afya hadi hapo ofisi ya takwimu itakapotoa viashiria vingine kwa kushirikiana na wadau wote wa ndani na nje ya nchi.

“Matokeo ya utafiti yameendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, lakini kwa upande wa malaria imeongezeka kutoka asilimia 7 mwaka 2010 mpaka asilimia 14 mwaka huu,” alisema Dk Chuwa.