Kihamia adai kudhalilishwa

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Muktasari:

Kihamia alitoa ‘mashtaka’ hayo jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) alipoomba nafasi ya kufafanua hoja zilizotolewa na Lema na Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro kuwa hawezi kutoa uamuzi hadi apate ushauri kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Arusha. Mkurugenzi wa Jiji, Athuman Kihamia amedai kuwa mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kwa tiketi ya Chadema amemdhalilisha kwa kudai  ‘ameolewa na mkuu wa mkoa huo’, Mrisho Gambo.

Kihamia alitoa ‘mashtaka’ hayo jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) alipoomba nafasi ya kufafanua hoja zilizotolewa na Lema na Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro kuwa hawezi kutoa uamuzi hadi apate ushauri kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Katika kikao hicho ambacho Lema, Lazaro na Gambo walihudhuria, Kihamia amesema mbunge huyo alimdhalilisha Oktoba 19 katika kikao cha kamati ya mipango miji.

Mkurugenzi huyo amesema kauli hiyo ilimdhalilisha sana mbele ya watumishi wake, lakini ameamua kuwasamehe na ataendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Hata hivyo, Lema amesema Baraza la madiwani liliagiza kuondolewa kwa wamachinga katikati ya mji, kubomolewa nyumba zilizojengwa katika maeneo yaliyovamiwa eneo la Block J, lakini hakuna utekelezaji.