Kihamia ampa siku saba Mbowe kumwomba radhi

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Athuman Kihamia akizungumza na wanahabari leo

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema amepewa siku saba kumuomba radhi Mkurugenzi  wa Uchaguzi, Dk Athuman Kihamia kutokana na kauli na kejeli dhidi yake.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Dk Athuman Kihamia amempa siku saba Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumuomba radhi kutokana na kauli na kejeli alizozitoa dhidi yake.

Kihamia ametoa msimamo huo, leo Alhamisi Septemba 20, 2018 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa marudio wa majimbo ya Monduli, Ukonga na kata 23.

Amesema Mbowe akiwa katika mkutano na wanahabari jana alitoa shutuma kwa Nec huku shutuma nyingine zikimlenga yeye (Kihamia) moja kwa moja.

Dk Kihamia amedai katika mkutano huo Mbowe alisema wakurugenzi wa halmashauri ni makada wa CCM huku polisi wakitumika na mkurugenzi wa uchaguzi anaujua mchakato huo lakini amekaa kimya.

"Namwambia (Freeman) Mbowe achague maneno ya kuongea yeye ni kiongozi mkubwa wa chama. Achuje maneno yake na awe na ushahidi, mimi sipendi kulumbana na wanasiasa na asitafute kiki,” amesema.

"Mimi sijawahi kukutana naye, lakini nimeshawaambia kina (John) Mnyika na John Mrema wamfikishie ujumbe, mimi si wa kutania," ameongeza.

Dk Kihamia amesema Mbowe asipoomba radhi basi Watanzania wawe makini kutokana na kauli zake.

"Kama alikuwa anatesti mitambo kuwa akitukana hajibiwi, mimi sipo hivyo lazima nitakujibu kwa sababu nipo kwa ajili ya kuhakikisha Nec inajizatiti kutekeleza majukumu yake"

Kwa mujibu wa Kihamia malalamiko yaliyotolewa na Mbowe hayana ukweli na kwamba Nec ilisimamia taratibu na sheria katika uchaguzi huo.