Kiini cha hamahama hiki hapa

Muktasari:

  • Wengi wanaohama upinzani kwenda CCM wamekuwa wakisema ni kutokana na upande huo kushindwa kupambana na ufisadi, hoja ambayo inaelezwa na wachambuzi kuwa haina ukweli.

 Wakati kukiwa na wimbi la wanasiasa kuhamahama vyama, wachambuzi wa kisiasa wamesema wengi wanasukumwa na masilahi binafsi badala ya masuala ya sera na itikadi.

Wengi wanaohama upinzani kwenda CCM wamekuwa wakisema ni kutokana na upande huo kushindwa kupambana na ufisadi, hoja ambayo inaelezwa na wachambuzi kuwa haina ukweli.

Katika kuzungumzia hilo, wanasema mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila akiwa upinzani alipinga ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kushinda, hivyo kuhoji iliwezekanaje wakati huo na sasa ishindikane.

Kwa wiki hii, upinzani umeondokewa na wanasiasa saba ambao baadhi wamerudi CCM na wengine hadi wamefikia uamuzi wa kuhama wamefanya hivyo zaidi ya vyama viwili.

Kafuli aliyekuwa Chadema akaenda NCCR-Mageuzi, akarudi Chadema, juzi alitangaza kuhama upinzani na huenda akajiunga CCM.

Wengine ni Samson Mwigamba aliyekuwa Chadema, ACT-Wazalendo na sasa amejiunga CCM; Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa CCM- Chadema- ACT- Wazalendo sasa karudi CCM.

Pia, Patrobas Katambi kutoka Chadema kahamia CCM. Lazaro Nyalandu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini alijiondoa CCM na kujiunga Chadema mwezi mmoja uliopita.

Mratibu wa mtandao wa kutetea haki za binadamu, Onesco ole Ngurumwa alitoa sababu mbili ambazo zinasababisha kuhama kwamba ni kutekeleza mambo ya kisiasa ambayo muhusika aliona hayaendi sawa au ni masilahi binafsi.

“Uhamaji huo, unajiuliza wanahama lini na saa ngapi. Ukiona mtu amehama zaidi ya mara mbili au tatu kwenda kwingine hatafuti malengo ya kisiasa kama sera na itikadi bali ni masilahi binafsi wameona mambo hayaendi vizuri,” alisema Ole Ngurumwa.

Alisema ukiona mtu anahama, anaacha ubunge ambao una fursa kubwa, una mamilioni ya fedha, huyu anakuwa ameshinikizwa na sababu ya kwanza ya malengo ya kisiasa na si masilahi binafsi na wanatoa sababu ya ufisadi ambayo itaeleweka kwa jamii.

“Labda, Kafulila anayesema suala la ufisadi, hivi mbona yeye alipigana Escrow hadi akashinda akiwa upinzani? Suala la Buzwagi na kashfa zingine, zimeibuliwa na upinzani, atusaidie anamaanisha nini kusema upinzani hauwezi kushughulikia ufisadi,” alihoji Ole Ngurumwa

Kauli hiyo imetolewa pia na Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala aliyesema, “Wengi wanaohama unaweza kuwaita ni ‘opportunist’, watu wanaangalia upepo unakwendaje na wao wanafuata na hao ni wengi hasa kipindi hiki.”

“Hawataua upinzani ila wanaweza kuudhoofisha, wanapaswa kukaa sehemu moja. Mtu kama Kafulila utampimaje? Upinzani haupiganii ufisadi pekee bali hata ujenzi wa demokrasia ambao tunauona wanaufanya,” alisema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuhama au kubadili chama cha siasa si jambo geni katika siasa na ni haki ya Kikatiba ya Mtanzania yeyote kufanya hivyo.

Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini alisema wao wataendelea kujenga vyama kama taasisi muhimu za maendeleo katika nchi na kamwe hawawezi kuruhusu nchi ikawa na chama kimoja.

“Ni dhahiri kuwa chama kuondokewa na wanachama wake si jambo jema, lakini ukitazama watu wanaohama vyama ni wanasiasa walewale wa siku zote na walikuwa kwenye vyama vingine kabla na kuhamia vyama wanavyotoka sasa,” alisema Zitto.

“Kwangu mimi kuna somo moja kubwa nalo ni kuandaa aina mpya ya wanasiasa, wanasiasa wanaojengwa kwenye itikadi na misingi. Kazi kubwa iliyopo mbele yangu kama kiongozi ni kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa kisiasa wajamaa.”

Aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), John Seka alisema, “Ukiwasikiliza wengi wanatoa sababu hiyo ya ufisadi na ndio sababu zao lakini ukichunguza zaidi unaweza kukuta ni njaa.”

Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo, Khamis Mgeja alisema madai kuwa upinzani hauwezi kupambana na ufisadi haya msingi wowote na wanapaswa kutoa sababu zinazoelekewa.

“Upinzani hauna mgambo, hauna magereza, hauna polisi, hauna chombo chochote cha dola, kazi moja wapo ya upinzani ni kuonyesha njia, kusema ule pale ufisadi na hata huo wanaosema unashughulikiwa si ni matunda ya upinzani,” alisema Mgeja aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamia Chadema

Mgeja alisema katika siasa suala la kuhama kutoka chama kimoja na kwenda kingine ni la kawaida, lakini tatizo linakuja pale zinapotolewa sababu zisizokuwa na tija ukilinganisha na hali halisi ya maisha ilivyo.

“Uchumi unasumbua, wananchi wanalia njaa, biashara zinafungwa, wanafunzi wanakosa mikopo, badala tujielekeze huko kutatua matatizo haya lakini tumeshindwa na kuanza kucheza sarakasi za kuwahamisha watu,” alisema Mgeja.

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akihutubia mkutano wa kampeni Mtwara Mikindani alisema wapinzani wasipoteze muda wa kumsubiri kuwa atahama CCM.

Kauli kama hiyo aliwahi kuitoa kupitia akaunti yake ya Twitter akisema, “Chama cha siasa ni itikadi, itikadi ni imani. Siamini sana katika kubadili imani kienyeji. Nitashughulikia mapungufu nikiwa ndani si nje.”

Hata hivyo, Mwigamba alisema, “Yale ambayo tulikuwa tunayapigania nikiwa ACT-Wazalendo yanafanywa na Rais Magufuli, na ACT-Wazalendo imeshindwa na ndio sababu za mimi kuamua kuhamia CCM.”