Kiini cha kilio cha Dangote chatajwa

Aliko Dangote

Muktasari:

Hatimaye kiini cha malalamiko ya Dangote Tanzania iliyoko mkoani Mtwara kimewekwa wazi kuwa ni hatua ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuiuzia kampuni hiyo gesi kwa bei kubwa sawa na kampuni zilizoko nje ya mkoa huo.

Dar es Salaam. Hatimaye kiini cha malalamiko ya Dangote Tanzania iliyoko mkoani Mtwara kimewekwa wazi kuwa ni hatua ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuiuzia kampuni hiyo gesi kwa bei kubwa sawa na kampuni zilizoko nje ya mkoa huo.

Kampuni ya Dangote ilikuwa inataka iuziwe gesi hiyo kwa Dola za Marekani kati ya tatu (Sh6,510) na nne (Sh8,680) kwa kila futi za ujazo 10,000 lakini TPDC imeng’ang’ania Dola 5.14 (Sh11,153.8) kwa wateja wote bila kujali kama yupo Mtwara au Dar es Salaam.

Hoja ya Dangote ni kwamba iko karibu na inapotoka gesi hiyo hivyo kuuziwa gesi kama vile imesafirishwa kutoka mbali si sahihi. Kampuni hiyo inadaiwa imekubali kununua gesi kwa bei ya TPDC kwa ajili ya umeme wa kawaida lakini imegoma kununua bidhaa hiyo kwa ajili ya kuzalisha saruji.

Akifafanua suala hilo katika mkutano wa waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapulya Msomba alisema tangu mwanzo walikuwa wanashindwa kufikia mwafaka na kampuni hiyo kwa sababu hawakubaliani na bei hiyo hata baada ya kuwashauri mara kadhaa watumie gesi badala ya mafuta.

Msomba alitaja sababu ya kutotaka kuipunguzia bei kampuni hiyo kuwa inatokana na mteja mkubwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kununua kwa Dola 5.14, hivyo hawawezi kushuka chini ya hapo, ingawa amekiri kuwa bado mazungumzo yanaendelea.

“Amekubali kununua gesi ya umeme kuanzia jana na atalipa kiasi hicho cha dola 5.14,” alisema Msomba.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema mazungumzo yanaendelea kati ya mfanyabiashara huyo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Mwijage alisema gesi ikichimbwa na kusafishwa gharama yake ni Dola tatu, ambayo kimsingi kampuni hiyo haina tatizo nayo, ila tatizo ni ongezeko la Dola 2.14 (Sh4,643.8) linalotokana na gharama za usafirishaji.

Alisema kampuni hiyo inataka gharama ipunguzwe kwa madai ipo karibu na kisima angalau ilipe Dola nne, jambo ambalo halijafikiwa mwafaka kati yao na TPDC ambao ndiyo wauzaji wa gesi.

“Ndiyo maana tulimsisitiza kutumia gesi, hizi gharama anazopata sasa za mafuta kama angetumia gesi zisingekuwepo,” alisema Mwijage.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari wiki hii, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Harpreet Duggal alisema kiwanda hicho kimesitisha uzalishaji kutokana na hitilafu za mitambo lakini pia alilalamikia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na matumizi ya jenereta za dizeli.

Baada ya Duggal kutoa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk Dalaly Kafumu alisema ni muhimu Serikali ya Awamu ya Tano ikalishughulikia kwa makini na kwa haraka suala hilo kwa sababu nchi inahitaji viwanda vijengwe ili iwe nchi ya viwanda.

Alisema Serikali ya Awamu ya Nne pamoja na mambo mengine, ilikiahidi kiwanda hicho kupata ardhi na malighafi ya madini ya chokaa kwa ajili ya kuzalisha saruji kupatikana kwa gharama nafuu na pengine bure.

“Nikiwa Kamishna wa Madini wakati ule, tulishirikiana na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuipa Dangote leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini ya chokaa zilizokuwa zinamilikiwa na Stamico... Ahadi pia ilitolewa kukipa kiwanda cha Dangote nishati ya umeme wa bei nafuu kwa kuiuzia gesi na makaa ya mawe kwa bei nafuu na pia uwezekano wa kutoa umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa kwa gharama nafuu. Kwa mazingira hayo kiwanda kilijengwa,” alisema.

Pia, mbunge huyo wa Igunga alisema ni wajibu wa Serikali kukutana na mdau huyo muhimu pamoja na wengine wa sekta ya saruji; gesi, makaa ya mawe; na taasisi na mamlaka za Serikali zinazosimamia sekta hizo kuweka utaratibu utakaoiwezesha Dangote kutumia makaa ya mawe, gesi na umeme wa gridi kutoka Tanzania bila kuongeza gharama zake za uzalishaji ili kiwanda kiendelee kupata faida.

Waziri Mwijage akijibu hoja za Dk Kafumu alisema malighafi ya chokaa inayosemekana aliahidiwa Dangote anayo na ana leseni ya kuchimba na ardhi wanayo ya kutosha. Kuhusu makaa, Mwijage alisema yapo ya kutosha tena kwa bei nafuu na kwamba awali yalikuwa yanauzwa kwa Dola 45 sasa ni Dola 35, wakati Afrika Kusini walikokataza yasiingizwe yanauzwa Dola 83 kwa bei ya wiki iliyopita.

 

Uzalishaji saruji

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuna viwanda 12 vya saruji; Lucky, Twiga, Camel, Rhino, Mbeya, Tanga, Arusha, ARM, Moshi, Kisarawe, Fortune na Dangote. Uwezo wa viwanda hivyo ni kuzalisha tani 10.3 milioni lakini vinazalisha tani 7.1 milioni na soko la ndani linahitaji tani nne milioni kwa mwaka na inayobaki inauzwa nje ya nchi.