Kijiji kinara kwa kilimo cha bangi nchini

Muktasari:

Ekari 32 kati ya 34 za bangi zilizofyekwa hivi karibuni nchi nzima, ni kutoka katika eneo hilo tu katika kipindi cha Januari hadi Februari.

Dar es Salaam. Ni sifa kubwa kwa kijiji kutambulika kwa kulima korosho, mahindi au mazao mengine ya biashara, lakini hali ni tofauti kwa Kijiji cha Lengilong, kilichopo katika Kata ya Engaroni, Wilaya ya Arumeru, Arusha. Hiki kinaongoza nchini kwa kulima dawa za kulevya aina ya bangi.

Ekari 32 kati ya 34 za bangi zilizofyekwa hivi karibuni nchi nzima, ni kutoka katika eneo hilo tu katika kipindi cha Januari hadi Februari.

Hayo yalielezwa jana na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA).

Kamishna wa Opreresheni (DCEA), Luteni Kanali Frederick Milanzi alitaja sababu za kijiji hicho kuongoza katika kilimo hicho kuwa ni kuwapo kwa wafadhili ambao ni wafanyabiashara wakubwa kutoka Kenya wanaoingia makubaliano na wanakijiji kuwa watanunua dawa hizo za kulevya.

Milanzi alitaja sababu nyingine ya kijiji hicho kulima bangi kwa wingi kuwa ni jiografia yake, akisema kipo katika mpaka wa Namanga (Kenya na Tanzania) na wakulima wengi wanategemea wanunuzi kutoka Kenya.

“Operesheni yetu tuliwalenga wakulima wanaowezeshwa na wafanyabiashara wa Kenya. Baadhi yao walikamatwa na magunia mbalimbali wakijiandaa kuyasafirisha kwenda nchini humo.

“Wakulima hao wanapeleka bangi nchini Kenya kwa wingi kwa kuwa ni karibu na mji wa Namanga. Wanasafiri haizidi kilomita 70 kwa kutumia pikipiki huku wakitumia njia za panya na huwaoni wakizipeleka bangi Arusha mjini wala Dar es Salaam kwani ni mbali,” alisema Milanzi.

Oktoba mwaka jana, mamlaka hiyo ilikamata magunia zaidi ya 2,300 ya familia 30 katika kijiji hicho yakiwa tayari kusafirishwa kwenda Kenya.

Kamishna Milanzi alisema Februari 26, mamlaka hiyo ilikwenda kwenye kijiji hicho na kubaini kuwa ekari zaidi ya 10 zimelimwa bangi na walikuta magunia matano ya mbegu na vyote viliteketezwa.

Aliyataja maeneo mengine ambayo ni sugu kwa kilimo cha bangi wilayani humo kuwa ni kata za Ingeraoni, Mukarashi na maeneo machache ya Kisimili Juu.

Kadhalika, Februari 27, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa, Oljoro walibaini ekari 24 za mashamba ya bangi ambazo ziliteketezwa, “Pia tulikuta magunia matatu ya mbegu za bangi katika Kata ya Mukarashi huku ekari tatu za bangi zikiteketezwa Kata ya Kisimil.”

Milanzi alisema kampeni inayofuata ni ya kuteketeza mirungi katika wilaya za Same, Tarime na Lushoto.

Sababu nyingine ya kushamiri kwa kilimo hicho katika maeneo hayo ni miundombunu yake kwani Milanzi alisema changamoto wanazokumbana ni ugumu wa kuyafikia.

Watanzania wanaswa na

‘unga’ wa Sh2 bilioni Kenya

Wakati DCEA ikibainisha hayo, Watanzania watatu wamekamatwa jana nchini Kenya wakidaiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroini zenye thamani ya Sh 1.9 bilioni.

Watuhumiwa hao ambao majina yao hayakutajwa, walinaswa wakiwa katika hoteli moja mjini Mombasa huku dawa hizo zinazodaiwa kuwa na uzito wa kilo 30, zikiwa zimefichwa katika nguo zilizowekwa kwenye mabegi.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya, polisi walikuwa wakijiandaa kuwafikisha mahakamani.

Lilieleza kuwa Watanzania hao waliingia nchini humo kwa usafiri wa basi wakitumia mpaka wa Lunga Lunga.