Kikao cha Lowassa chazuiwa Bukoba

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Muktasari:

Uamuzi huo wa polisi umekuja wakati tayari amri ya kuondoa zuio la mikutano ya ndani imetangazwa juzi hivyo kukiuka agizo hilo.

Bukoba. Jeshi la Polisi mkoani Kagera limezuia kikao ambacho kingemshirikisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyefika mjini hapa kuwafariji watu walioathirika na tetemeko la ardhi.

Uamuzi huo wa polisi umekuja wakati tayari amri ya kuondoa zuio la mikutano ya ndani imetangazwa juzi hivyo kukiuka agizo hilo.

Lowassa alikuwa katika ziara ya siku moja mkoani hapa jana kuwafariji waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10 na kuua watu 17 na wengine 253 kujeruhiwa huku likibomoa zaidi ya nyumba 840.

Mbali na kufariji waathirika, Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alipangiwa kukutana na viongozi wa chama hicho wa ngazi mbalimbali wilayani Bukoba, lakini Jeshi la Polisi lilimzuia licha ya kutangaza juzi kuwa limeondoa amri ya kuzuia mikutano ya ndani.