Mgomo wa daladala Tanga wafikia ukomo

Muktasari:

  • Usafiri wa daladala kurejea kama kawaida kesho Jumatano.

Tanga. Mgomo wa daladala uliolitikisa Jiji la Tanga kwa siku mbili umemalizwa baada ya viongozi wa Muungano wa Wasafirishaji Tanga (Muwata), Jeshi la Polisi na wadau wa usafirishaji kufanya kikao kwa zaidi ya saa nne.

Kikao hicho kimefanyika leo Jumanne Oktoba 17, 2017 chini uenyekiti wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Daudi Mayeji, viongozi wa baraza la ushauri la Sumatra na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga.

Makubaliano manane yamefikiwa kwa mujibu wa Ofisa wa Sumatra Mkoa wa Tanga, Dk Walukani Luhamba.

Amesema makubaliano hayo yamefikiwa kuhusu utozaji wa faini uliolalamikiwa na wenye daladala kwamba unavuka viwango, uchambuzi wa makosa yanayotozwa faini, vituo kutokuwa na mabango kutokana na halmashauri kutolielekeza Jeshi la Polisi, ushuru wa jiji kutozwa faini kila siku, ujazaji wa abiria mabasi ya mjini, kuomba mashine za elektroniki, sare za madreva na makondakta na muda wa kisheria wa kulipa faini.

Ofisa huyo amesema katika kikao hicho wameafikiana kuwa sheria ni lazima ifuatwe na Jeshi la Polisi na Sumatra hawatasita kuchukua hatua kwa watakaokiuka.

Godfrey Julius ambaye ni dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Magomeni na Raskazone amesema mgomo umekwisha na kwamba utoaji huduma utaanza kesho asubuhi.

"Viongozi wetu wametueleza kwamba kero zetu zinafanyiwa kazi, lengo letu lilikuwa ni kufikisha ujumbe na umefika, hivyo kesho asubuhi tutaingia barabarani kutoa huduma," amesema.