Profesa Anangisye amrithi Mukandala UDSM

Muktasari:

Profesa Mukandala amemaliza muda wake wa uongozi.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete amemteua Profesa William-Andey Anangisye kuwa makamu mkuu wa chuo hicho.

Uteuzi huo umeanza leo Jumanne Desemba 5,2017 ikiwa ni siku ya mwisho ya Profesa Rwekaza Mukandala wa kumaliza muda wake wa uongozi katika wadhifa huo.

Taarifa ya uteuzi huo iliyotolewa na UDSM imesema, “Uteuzi huu ni wa miaka mitano kuanzia leo Desemba 5.”

Kabla ya uteuzi wake, Profesa Anangisye  alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce) tangu Machi 2015.

Kabla ya kuanza kufundisha elimu ya juu, kwa miaka 11 kati ya mwaka 1988 na 1999, alikuwa mwalimu wa sekondari za Iyunga, Tambaza na Mkwawa.

Kufika alipo, alijiendeleza kutoka diploma ya ualimu aliyohitimu mwaka 1988 na kupata shahada ya kwanza mwaka 1992 na miaka mitano baadaye alihitimu shahada ya uzamili zote UDSM.

Mwaka 2006 alipata Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Edinburg, Scotland.