Kikwete amwambia VC mpya UDSM akili za kuambiwa achanganye na zake

Muktasari:

Kikwete alimsisitizia Profesa Anangisye kuwa hana haja ya kutengeneza maadui katika majukumu yake hayo mapya na ili afanikiwe ni muhimu akafanya kazi na watu wote. “Huna sababu ya kutengeneza maadui, fanya kazi na watu wote na umchukilie kila mmoja jinsi alivyo halafu baada ya hapo utajua nani ni nani na sio kusikiliza maneno ya watu, ndiyo maana unaambiwa akili za kuambiwa changanya na zako,”

       Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jakaya Kikwete amemwambia makamu mkuu mpya wa chuo hicho Profesa William Anangisye kuwa akili za kuambiwa achanganye na za kwake hivyo asisikilize maneno ya watu na badala yake afanye kazi na wote.

Kikwete alimsisitizia Profesa Anangisye kuwa hana haja ya kutengeneza maadui katika majukumu yake hayo mapya na ili afanikiwe ni muhimu akafanya kazi na watu wote. “Huna sababu ya kutengeneza maadui, fanya kazi na watu wote na umchukilie kila mmoja jinsi alivyo halafu baada ya hapo utajua nani ni nani na sio kusikiliza maneno ya watu, ndiyo maana unaambiwa akili za kuambiwa changanya na zako,”

Kikwete ambaye pia ni rais mstaafu wa awamu ya nne aliyasema hayo wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala ambaye alishika nafasi hiyo tangu mwaka 2006.

Hafla hiyo ilikwenda sambamba na kusimikwa kwa Profesa Anangisye aliyetuliwa rasmi kuchukua nafasi hiyo Desemba 5.

Alisema, “Lengo letu ni kuona chuo hiki kinakuwa bora zaidi ndani na nje na nina imani kutokana utendaji na umahiri wako hilo litawezekana kwa sababu nina uhakika tumeshafanya uamuzi sahihi kukuchagua katika nafasi hii.”

Kikwete pia alimpongeza Profesa Mukandala kwa maendeleo makubwa ambacho chuo hicho imekipata wakati wa uongozi wake.

“Wote tunatambua kazi nzuri aliyoifanya Profesa Mukandala ukiangalia kilivyokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam cha mwaka 2006 sio sawa kabisa na kilivyo leo, tunashukuru kwa kujitoa na kupeperusha vyema bendera ya chuo hiki,”

Kwa upande wake Profesa Anangisye aliahidi kuendeleza kazi nzuri iliyoachwa na Profesa Mukandala ili kuhakikisha chuo hicho kinakuwa miongoni mwa vyuo bora zaidi Afrika.

Profesa Anangisye aliomba ushirikiano wa walimu, watumishi na wanafunzi wa chuo hicho katika utendaji wake wa kazi na kueleza kuwa peke yake hataweza kufanikiwa kutimiza lengo hilo pasipo ushirikiano wao.