Kikwete kuzindua chama cha watanzania waliosoma Marekani

Muktasari:

Chama hicho kinawakutanisha pamoja Watanzania hao ili kuishirikisha jamii umuhimu wa kusoma na kurudi nyumbani kufanya kazi

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya Nne,  Jakaya Kikwete kesho Julai 21, 2018 anatarajiwa kuzindua chama cha Watanzania waliopata fursa ya kusoma Marekani kupitia udhamini unaotolewa na Taasisi ya Africa-America (AAI) iliyopo nchini humo.

 

Chama hicho kinawakutanisha pamoja Watanzania hao ili kuishirikisha jamii umuhimu wa kusoma na kurudi nyumbani kufanya kazi,a wanahamasisha watu mbalimbali hasa vijana kutafuta fursa za kusoma kisha kutumia elimu hiyo kuisaidia jamii.

 

Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 20, 2018 mwenyekiti wa chama hicho, mhandisi  August Kowero amesema chama hicho kinalenga kuwakutanisha watu wote waliowahi kupata fursa ya kusoma Marekani ili kuhamasisha na wengine.

 

"Watu wengi tulipata fursa ya kusoma Marekani lakini wengine walibaki huko huko, sisi tukarudi. Tumeona tukiwa nyumbani tuanzishe taasisi yetu  itakayotuweka pamoja," amesema Mwenyekiti huyo na kubainisha kwamba kwa sasa wamefika wanachama 117.

 

Amesema zaidi ya Watanzania 1,200 walipata fursa ya kusoma marekani kupitia mradi huo tangu mwaka 1961,  AAI ilipoanza kudhamini masomo kwa Watanzania.

 

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa chama hicho mchungaji Isaac Chengula amesema AAI ni taasisi iliyoanzishwa mwaka 1953 kwa lengo la kuwajengea uwezo waafrika ili wakabadilishe maisha katika jamii zao.

 

Amesema mpaka sasa waafrika zaidi ya 15,000 wamepata fursa ya kwenda kusoma Marekani na wengi wao sasa ni viongozi, wafanyabiashara na wanafamilia wazuri.

 

"Sisi ni baadhi tu ya waliopata fursa ya elimu Marekani, tumeona tuanzishe chama ili kuwavuta na wengine kuja kujumuika nasi. Tunafurahi kwamba kesho tunazindua chama chetu na mgeni rasmi atakuwa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete," amesema Chengula.