Kila aliye karibu na staa anataka kuimba

Muktasari:

Wanamuziki wa sasa wanabadilika nywele na mavazi tu. Lakini kinachofanyika jukwaani ni kile kile alichokifanya Inspekta Haroun miaka 17 iliyopita.

Hakurudi Tanga. Akafuate nini? Mwili wake ulikuwa na thamani ya shoo kadhaa za Alikiba. Sura yake wauaji wa Kibiti wakiiona wanaokoka hapo hapo bila kusubiri maneno ya Mzee wa Upako wala Gwajima. Mzuri mpaka uzuri wenyewe unaona wivu juu yake.

Amwachie nani bata za viwanja vya Daslama mjini? Ndio kwanza alikuwa ameanza kuonja ladha ya utamu wa Jiji? Rafiki aliyeishi Tabata, ambaye alianza kujitegemea baada ya kupita njia alizopitia yeye, akampokea kisha akamuhifadhi.

Ghetto lenye kila kitu ndani kinachotakiwa kwa mtoto wa kike wa mjini. Maana kuna mtoto wa kike na mtoto wa kike wa mjini. Kilivutia kuliko sura na shepu za mastaa wengi wa Bongo Movie. Kuna vyumba vya watoto wa kike vina urembo kuliko warembo wenyewe. Ndo hiki alichohifadhiwa.

Haya yote yanakuja baada ya Nasra kufukuzwa nyumbani kwa dada yake, (siyo tumbo moja ila wanatoka sehemu moja Chumbageni Tanga) ambaye alimleta Daslama kumsaidia shughuli zake za Saloon. Haukupita mwaka kabla ya kuanza kuraruana kwa sababu za kipuuzi.

Nasra aliingia Dar kama msichana wa kawaida sana. Mitoko na pamba za kijanja alizoiga kutoka kwa wateja wa saloon ya dada ghafla akawa kiumbe pendwa. Wateja wa wakageuka madalali wa mwili wake. Aliuzwa kama njugu, na huduma yake ilikuwa siyo ya nchi hii. Kila pedeshee akataka kummiliki.

Akaanza kutishia himaya ya mwenyeji wake (dada mtu). Mwanamke aliyempokea Tabata ni miongoni mwa wateja wa saloon ya dada yake, ambaye pia alishiriki sana kumkuwadia Nasra. Mrembo ni rahisi kumjua mrembo mwenzake. Akampokea kwa bashasha la kike akijua kuwa sasa atavuna pesa za ukuwadi kwa uhuru zaidi.

Ungewatembelea mchana muda wote wamelala, sura zao zimekunjamana kwa ukosefu wa usingizi. Nyakati za jioni wakiwa wamejipara, ukiwaona utashangaa matajiri wote hapa mjini wamekosaje kuolewa? Okay sawa waoaji hawapo, na ‘mabarazameni’ hawa wanaooa na kuzalisha wanawake wa nje ya Bongo hawawaoni hawa kina Nasra?

Jioni ya Jumanne iliyopita, niliitwa na mshikaji wangu mmoja hivi mitaa ya Goba katika baa moja maarufu sana maeneo yale. Kwa kuwa kesho yake ilikuwa sikukuu kwanza nilishukuru kukumbukwa na rafiki, pili sikusita kwenda maana kesho yake yalikuwa mapumziko. Nikatimba haraka sana kana kwamba nimeitwa Ikulu.

Nikamuona mshikaji mmoja mrefu, mnene, kasimama kaunta akinunua vinywaji kwa fujo kuliko mtu mwingine yeyote. Wasichana wengi waliomzengea walipewa bia na kufukuzwa pale alipo. Nilivyosogea zaidi ndipo nikajua kuwa anayefanya fujo zile ni mshikaji wangu niliyemfuata.

Maisha ya kibwegebwege hayo sijazoea na siyapendi. Kwanza sina marafiki wa kindezi mamna hiyo. Sikutamani tena kuonana naye wala kuonekana na marafiki wengine wanaonijua. Nikaenda kukaa kivyangu kwenye kona ambayo ni wahudumu tu walioniona. Eneo nililokuwepo niliweza kumuona vyema mshikaji akiendelea na undezi wake. Katika kutupatupa macho nikamuona Nasra. Huyu msichana watoto wa mjini wengi wanamjua nami namfahamu kama miongoni mwa wasichana wanyonya damu. Nasra hakuwa mtu wa kuomba bia, yeye huitwa au kufuatwa.

Nasra alikuwa kakaa kando kidogo ya mshikaji akiwinda na hakukosea, kwani mshikaji niliyemfuata baada ya kukutanisha macho na Nasra hakutaka hata salamu akaanza kuagiza apelekewe anachotaka. Nasra alikuwa ni zaidi ya jini mbele ya macho ya mwanaume. Mimi nilikuwa kando natazama mchezo wote.

Nasra akaanza kuletewa bia, oda ya mshikaji huyo. Dakika chache baadaye tayari walikuwa wamekaa pamoja, tena mshikaji ndiye aliyemfuata Nasra pale alipo. Kwenye runinga walionesha tamasha moja kubwa la muziki lililofanyika hivi karibuni, likiwa limewakutanisha wanamuziki wengi sana wa Bongo Fleva. Angalau nilipata kitu cha kunisahaulisha ujinga wa mshikaji. Nilimuacha anyonywe damu na Nasra mpaka mhogo aseme mhoho.

Baada ya kero ya mshikaji wangu ikaja kero nyingine ambayo ni bora ile kero ya mshikaji. Nikapikicha macho ili niwe na uhakika na ninachotazama. Kwamba ni shoo ya leo (siku hiyo) au ni shoo ya miaka 15 iliyopita? Wasanii wapya jukwaa jipya, lakini swaga mbona za kale?

Wanamuziki wa sasa wanabadilika nywele na mavazi tu. Lakini kinachofanyika jukwaani ni kile kile alichokifanya Inspekta Haroun miaka 17 iliyopita. Tena yawezekana LWP walikuwa bora zaidi kwa sababu hawakuiga swaga za Juma Nature, kuliko hawa ambao wanafanya alichofanya Nature miaka hiyo.

Kwenye jukwaa la Fiesta miaka 18 iliyopita Profesa Jay, akiwa tayari ana dakika 30 jukwani akivuta pumzi kabla ya kuendelea na shoo aliuliza mashabiki: “Tuendelee ama tusiendelee?” Swali lilienda sambamba na biti kurusha watu, mashabiki wakiitikia “Tuendelee.” Alikuwa akicheza na jukwaa kunogesha shoo.

Leo hii mwanamuziki kaimba wimbo mmoja wenye ‘vesi’ mbili tena fupi kama video za insta, tayari anaanza kuuliza mashabiki “Tuendelee ama tusiendelee?” Huu ni ‘uwaki’ wa kiwango cha lami. Mwanamuziki hajaanza hata kuimba wimbo tayari anawashurutisha mashabiki eti “Piga keleleeee.”

Hizo zilikuwa mbinu za nyakati zile kuamsha mizuka ya mashabiki. Wakati ule mwanamuziki anagonga nyimbo tano zenye ‘vesi’ tatu tena ndefu. Mashabiki wanasikiliza mistari kuliko midundo wala viuno, ndipo swaga za piga kelele au tuendelee ama tusiendelee zikaja.

Mashabiki wa kizazi hiki wagongee ngoma tu watapiga kelele na watataka uendelee ama usiendelee. Mambo ya “Upande huu siwasikii.” Mambo ya kale sana. Yanachosha maana yameshafanyika sana majukwaani toka enzi za kina Remmy Ongala.

Toka enzi za Dj Bonny Luv mpaka katika dunia ya kina Dj Tass, bado mwanamuziki yuko jukwaani anaanza kubishana na Dj, “Yo yo Dj gonga track number tatu.” Manaake mpaka anapanda jukwaani hakujiandaa. Kwenye ulimwengu ambao hautegemei CD tena.

Afande Sele alizidiwa pale Uwanja wa Uhuru 2004, akazimia jukwani baada ya kukaidi ushauri wa Daktari aliyemuonya asifanye shoo baada ya kugundua ana wadudu wa malaria kama wote. Leo hii eti Lavalava naye anazimia jukwaani baada ya kupigwa busu na shabiki wa kike. Busu lenyewe la utosini.

Hii inatokana na wanamuziki kukosa muda wa kujifunza kwa wenzetu. Wako bize kuchat na madem mitandaoni badala ya kutazama wenzao duniani wanafanya nini kwa sasa. Matokeo yake wanarudia alichofanya Stara Thomas maika hiyo. Jifunzeni.

Muziki sasa umekuwa kama kichaka cha watu waliofeli kila kitu. Mtu akifeli masomo anaona njia rahisi ni kufanya muziki. Akiachika au kukosa mume basi stress anahamishia kwenye muziki. Kila mtu anataka kuwa mwanamuziki bila kipaji wala karama.

Bongo Movie ilianza kutoweka na kuharibiwa wakati ule. Kina Kanumba walipotenda dhambi makusudi kwa kuwaaminisha watu kuwa msichana mrembo mwenye sura, shepu na jina mjini anafaa kuigiza. Wakaingiza wauza nyago kibao Kwenye tasnia ya filamu.

Kila mtu aliyepata umaarufu kwenye mambo mengine akaingizwa Kwenye filamu. Hapo ndipo sanaa ilipoanza kuyumba kwa kukosa wito kwa wasanii. Mtu aliyeozoea maisha ya kudanga mjini ni ngumu kumpotezea muda wake ‘lokeshini’ mwezi mzima.

Filamu zikaanza kutolewa ili mradi kuna sura ya msichana mzuri kwenye kasha last CD. Lakini ukitazama kazi yenyewe haina mbele nyuma wala kati. Ndicho kinachotokea kwenye muziki. Upuuzi umekuwa mwingi sana kama ilivyokuwa kwenye sanaa ya filamu.

Na sasa ugonjwa huu unasambaa kwenye viunga vya Bongo Fleva. Kosa siyo la wadau wa muziki. Kosa ni watu kuamini kuwa ukiwa karibu na mwanamuziki unaweza kuwa staa wa muziki. Usishangae kusikia House Girl wa Diamond kutoa singo kali mwisho wa mwezi huu.