Kilichojificha nyuma ya mabango ziara za viongozi

Rais John Magufuli, akisoma mabango yenye ujumbe mbalimbali  wakati wa mkutano wake wa hadhara uliofanyika Julay 22, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Muktasari:

Alisema hayo wakati kukiwa na ongezeko kubwa la wananchi kuibuka na mabango, hasa kwenye ziara za Rais John Magufuli, ambaye amekuwa akiyasoma hadharani na wakati mwingine kuagiza yapigwe picha ili ayasome baadaye na kuyafanyia kazi.

Dar es Salaam. Mapema wiki hii, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitaka wananchi wanaokwenda kwenye mikutano ya hadhara wakiwa wamebeba mabango, wasizuiwe na badala yake waachiwe wayanyooshe ili kueleza hisia zao.

Alisema hayo wakati kukiwa na ongezeko kubwa la wananchi kuibuka na mabango, hasa kwenye ziara za Rais John Magufuli, ambaye amekuwa akiyasoma hadharani na wakati mwingine kuagiza yapigwe picha ili ayasome baadaye na kuyafanyia kazi.

Kasi hiyo ya kuongezeka kwa mabango ilikuwa kubwa wakati Rais alipokuwa katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Magharibi, kiasi cha kuonekana kama vurugu mkoani Kigoma na mikutano iliyofuata mkoani Tabora, Rais aliwataka wasiyaonyeshe.

Na wakati fulani alisema, “hayo mabango yenu mkatandike kwenye vitanda vya wake zenu,” wakati walipoyanyoosha katika moja ya mikutano yake mkoani Tabora.

Vitendo hivyo vinaelezewa na wachambuzi wa siasa kuwa vinatokana na ama wananchi kutopata fursa ya kutoa maoni yao, au watendaji kutowajibika ipasavyo au tabia ya Rais Magufuli kuchukua hatua papo hapo.

“Kubanwa kwa demokrasia, kama kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kumewakosesha wananchi fursa kutoa maoni yao,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu).

“Huko nyuma, wananchi walipata fursa ya kutoa maoni yao, ingawa sasa utawala huu umeonyesha nia ya kutatua kero, kama alivyotoa ardhi kwa wananchi huko Tanga.

“Watu wamekosa fursa ya kutoa maoni yao katika mikutano ya hadhara, maandamano na makongamano, ndiyo maana wanapopata nafasi kama hiyo wanajitokeza kwa wingi.”

Alisema kutokuwapo kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kumewafanya wananchi kukosa fursa ya kutoa maoni na kero zao.

Hata hivyo, Profesa Mpangala alisema kitendo cha Rais kutatua matatizo ya wananchi pale anapoyasikia kinaweza pia kusababisha hali hiyo kuzidi kuongezeka. “Kero za wananchi zipo kwa muda mrefu na hiyo imetokana na kipindi cha ubepari mamboleo tangu miaka ya tisini ambako vitendo vya rushwa na ufisadi na kutolindwa kwa haki za watu vilikithiri,” alisema Profesa Mpangala.

“Rais Magufuli ameonyesha dhamira ya kupambana na madhambi hayo ndiyo maana wananchi wanamfuata na mabango yao.”

Serikali ilipiga marufuku mikutano ya hadhara na ya ndani mwaka jana, kabla ya kuruhusu mikutano ya wabunge, ikizuia wabunge kutoka maeneo mengine kuhudhuria nje ya majimbo yao.

Wananchi hunyoosha juu kwa bidii mabango hayo wakati viongozi wa juu wa Serikali wanapohutubia na huonekana kuwabughudhi au kutibua mtiririko wa hotuba zao, ambazo hulenga kueleza mikakati ya Serikali na mafanikio yaliyokwishapatikana.

Akiwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Julai 23, idadi ya wananchi waliovamia sehemu ya kati ya uwanja kujaribu kumkaribia Rais ili aone ujumbe wao ilikuwa kubwa.

Kitendo hicho kiliwafanya askari wakimbilie kuwazuia wasizidi kusogelea jukwaa, lakini Rais akawataka askari waachie wayanyooshe juu na yeye kushuka jukwaani kwenda kuyasoma.

Baadhi yalizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi, mirathi, kubambikiwa kesi, bomoabomoa, kutolipwa fidia na kunyang’anywa mashamba.

Baada ya kuyasoma, Rais aliwaambia wananchi hao kuwa atayashughulikia, lakini akasema mengine ni kutokana na kufuata sheria.

“Kama ubomoaji nyumba, hata mimi nabomoa kama umejenga kinyume cha sheria,” alisema Rais siku hiyo.

Hakurudia kuyasoma katika mikutano iliyofuata mkoani Tabora zaidi ya kuwahimiza wananchi wayashushe.

Hata hivyo, akiwa mkoani Tanga, Rais Magufuli alionyesha kukerwa na baadhi ya mabango yaliyolalamikia mishahara midogo wanayolipwa katika maeneo yao ya kazi, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Pongwe wakati akielekea Chongoleani kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda.

“Ndugu zangu niwaambie, mimi si mpole kiasi hicho, kama mnavyofikiria. Nasema kama mnaona mshahara ni mdogo, acheni kazi nendeni mkalime,” alisema Rais.

Matumizi ya mabango pia yameonyesha wananchi kutafuta suluhisho la kero zao sugu wakiamini kuwa viongozi hao ndiyo pekee wanaoweza kuwasaidia.

Hali kama hiyo pia ilitokea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa wilayani Sikonge, Tabora ambako alitaka wananchi waruhusiwe kuyaonyesha baada ya kuona askari wanawazuia.

“Siku nyingine msirudie na kuanzia sasa waacheni wananchi waonyeshe mabango yao kwa kuwa ndiyo njia wanayotumia kuonyesha hisia zao kwa yale wanayokumbana nayo na kuwasababishia kero,” alisema Majaliwa.

Mabango siyo tu yamekuwa yakitumika kwa viongozi hao wa juu, bali hata kwa viongozi wengine kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa Kamati Maalumu ya Bunge inayochunguza madini ya Tanzanite ilipofika Mererani katika machimbo hayo.

Moja ya mabango ambayo wananchi walibeba ni lile lililosema “Tuko tayari kulipa kodi kumsaidia Rais lakini tuangaliwe.”

Akizungumzia suala hilo mhadhiri mwandamizi wa sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema wananchi wengi wanamuona Rais kama tegemeo lao baada ya kukosa misaada wanayoitarajia kutoka kwa watendaji wa ngazi za chini.

“Rais kajipambanua kusaidia tabaka la watu wa chini na tabaka hilo linatambua hivyo. Kwa mantiki hiyo linachukua fursa hii ili kutatuliwa matatizo yao,” alisema Dk Makulilo.

“Watendaji wa ngazi za chini wameshindwa kuwasikiliza na kutoa ufumbuzi madhubuti kwa matatizo ya tabaka la chini. Hivyo tabaka hili linamuona Rais kama mkombozi wa wanyonge.

“Awamu ya tano na hususani, Rais amekuwa akitoa ufumbuzi wa haraka kwa matatizo. Rais hapendi kusikia lugha ya michakato.”