Thursday, October 5, 2017

Rahco yajichanganya suala la bomoabomoa Moshi, Tanga, Dar es Salaam

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi ebahemu@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Furaha waliyokuwa nayo baadhi ya wakazi wa Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam waliojenga pembezoni mwa njia ya reli huenda ikageuka simanzi baada ya Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kusema haina mpango wa kulegeza masharti ya umbali wa hifadhi katika mikoa hiyo.

Awali, wakazi wa Kilimanjaro na Tanga walifikisha vilio vyao kwa wakuu wa mikoa, ambao walitoa maagizo ya kutumika kwa busara na mazungumzo ili kufikia muafaka wa suala hilo, hofu yao ikiwa ni kubomolewa kwa kiasi kikubwa kwa miji yao endapo sheria hiyo itatekelezwa.

Wananchi wengi wanadai kuwa waliuziwa kihalali maeneo hayo na halmashauri za miji yao na wanazo nyaraka zote za kisheria zinazoonyesha uhalali umiliki.

Septemba 29, ofisa habari wa Rahco, Catherine Moshi alisema kampuni hiyo ilikubaliana na maombi hayo kwa kusema Tanga barabara nyingi zinakutana na reli hivyo wakifuata sheria hasara itakuwa kubwa.

“Kuna maendeleo mengi yamefanyika baada ya maeneo ya reli kuchukuliwa, huku baadhi ya halmashauri zikiuza maeneo ya reli. Siyo Tanga tu, Moshi pia tuliona tuache kutumia sheria hiyo. Hata Dar es Salaam kama tungeamua kubomoa maeneo ya Kamata wengi wangeathirika,” alisema Moshi.

Kutokana na hatua hiyo baadhi ya nyumba zilizokuwa zimewekea alama nyekundu ya X zilianza kupitiwa upya na kuandikwa  kwa rangi ya njano maneno yaliyosomeka ‘Imefutwa’.

Hata hivyo, katika tangazo lililotolewa katika gazeti hili jana, Rahco inasema bomoabomoa ya nyumba zilizopo katika hifadhi ya reli (mita 30 kila upande) katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam iko palepale.

Tangazo hilo lililoidhinishwa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa Rahco linasema kampuni hiyo itaendelea na mchakato wake wa kuwaondoa wavamizi wote wa hifadhi za reli nchi nzima, waliopewa notisi na kuwekewa alama ya X ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Reli inayozuia ujenzi ndani ya hifadhi njia ya reli.

“Rahco inakanusha uzushi unaoenezwa kuwa kuna mabadiliko ya upana katika hifadhi ya reli kwa baadhi ya mikoa,” linaeleza tangazo hilo.     

-->