Kilio cha Makonda kwa Sirro chajibu

Muktasari:

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa jeshi hilo limewakamata watu hao katika eneo la Kinondoni kwa tuhuma za kukutwa wakiuza shisha.

Dar es Salaam. Kilio cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa watu wanaojihusisha na uuzaji na uvutaji wa shisha hawakamatwi na polisi kimeanza kujibiwa, baada ya jeshi hilo kufanikiwa kuwanasa watu watatu.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa jeshi hilo limewakamata watu hao katika eneo la Kinondoni kwa tuhuma za kukutwa wakiuza shisha.

Sirro alisema jana kuwa alipewa taarifa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzane Kaganda kuwa waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na vielelezo hivyo.

“Operesheni inaendelea na leo (jana) Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni amesema wamewakamata watu hao wakiuza shisha, upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Sirro.

Akizungumza hivi karibuni mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwawakati akizindua mradi wa uboreshaji miundombinu ya umeme jijini Dar es Salaam, Makonda alisema biashara na uvutaji wa shisha bado unaendelea licha ya polisi kukanusha kuwapo kwa shughuli hizo.

Mkuu huyo wa mkoa pia aliwatuhumu polisi kuwalinda watu wanaojihusisha na shisha, akisema huenda wamekuwa wakipewa rushwa na wahusika.

Katika hatua nyingine, Sirro alisema limeibuka kundi la kihalifu katika eneo la Kariakoo kwenye mitaa ya Mkunguni na Sukuma ambalo linawapora raia wenye asili ya Kiasia na kuwafunga kamba.

Kamanda huyo alisema kuwa kundi hilo linapowaona raia hao wakiwa maghorofani huwafuata sehemu hizo na kuwafanyia unyama huo.

“Hili kundi linawavamia watu wenye asili ya Kiasia na huwa wanawavizia. Tumewakamata watuhumiwa wawili wakiwa na vifaa mbalimbali walivyoiba kabla hawajaondoka eneo la tukio,” alisema