Kim amwandikia barua Trump kuomba wakutane

Muktasari:

  • Viongozi hao walifanya mkutano wa kwanza wa kihistoria Juni nchini Singapore ambao ulileta matumaini ya kupata ufumbuzi wa kusitisha programu ya nyuklia ya Korea Kaskazini.

Washington, Marekani. Rais Donald Trump wa Marekani amepokea barua yenye “matumaini” kutoka kwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ikiomba ufanyike mkutano wa pili baina yao.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani ya White House, uratibu wa kikao hicho umeanza.
"Rais amepokea barua kutoka kwa Kim Jong Un. Ilikuwa barua ya upendo na mwelekeo chanya," msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Sanders aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu.
Sanders alisema ujumbe uliomo kwenye barua hiyo unaonyesha utawala wa Korea Kaskazini umeendelea kuzingatia makubaliano ya kuondokana na silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.
"Lengo la msingi la barua hiyo ni kupanga kikao kingine na Rais, jambo ambalo tuko wazi nalo na mchakato wa uratibu umeanza," alisema katika kikao hicho cha kwanza katika Ikulu baada ya karibu wiki tatu.
Sanders aliongeza kwamba, barua hiyo ilikuwa "ushahidi mzuri wa maendeleo” katika uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini.
Trump na Kim walifanya mkutano wa kwanza wa kihistoria Juni nchini Singapore ambao ulileta matumaini ya kupata ufumbuzi wa kusitisha programu ya nyuklia ya Korea Kaskazini.