Ndugu wa Bobi Wine akamatwa

Ndugu wa mwanamuziki Bobi Wine aliyegeukia siasa, Eddy Yawe.

Muktasari:

  • Bobi Wine amepitia Nairobi, Kenya na ndege inasemekana tayari imeondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kuelekea Uganda

Kampala. Saa chache kabla ya kuwasili kwa mbunge wa Kyadondo, Bobi Wine polisi imemkamata ndugu wa mwanamuziki huyo aliyegeukia siasa, Eddy Yawe.

Yawe amekamatwa na  vikosi vya usalama na kuzuiwa katika kituo cha polisi uwanja wa Entebbe akiwa pamoja na msemaji wa Chama cha Democratic, Alex Mufumbiro.

Walikuwa wamefika katika uwanja wa ndege wa Entebbe katika kile kilichofahamika ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya mbunge huyo ambaye anatarajiwa kurejea leo nchini Uganda, akitokea Marekani.

Duru za habari zinasema polisi wametahadharisha mkusanyiko wowote wa watu karibu na maeneo ya uwanja huo wa ndege na barabarani itokayo uwanjani hapo na kila mwanafamilia anayewasili uwanjani hapo anakamatwa.

Kwa sasa vikosi vya polisi mjini Kampala viko kwenye tahadhari kubwa kabla ya kuwasili kwa mbunge huyo wa Kyadondo East.

Bobi Wine anatarajiwa kuwasili Kampala leo Alhamisi kutoka nchini Marekani ambapo alikuwa ameenda kupata matibabu baada ya kuripotiwa kuteswa na vikosi vya usalama.

Tangu atangaze kurudi Uganda, makamanda wa polisi mjini Kampala wamekuwa wakifanya mikutano tangu Jumatatu kujiandaa kurudi kwa mbunge huyo.

Zaidi ya watu 1000 wanatarajiwa kufurika barabara ya Entebbe kumkaribisha Bobi ambaye ana wafuasi wengi vijana.