Marekani,China zapatana

Muktasari:

Maofisa wa ngazi ya juu kutoka pande zote wamekubaliana kuondoa vitisho vya ushuru na kufanya kazi kwa pamoja

Washington, Marekani. Marekani na China zimetangaza kusitisha vita vya kibiashara kati yao, baada ya kukubaliana kuondoleana vitisho vya ushuru na kufanya kazi pamoja kupata makubaliano mapya.

Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin na mshauri mkuu wa Rais Donald Trump kuhusu uchumi, Larry Kudlow wamesema maofisa wa nchi hizo mbili walifikia muafaka wa kuchukua hatua za kuondoa nakisi ya biashara baina ya nchi zao.

Baada ya mkutano uliofanyika mjini Washington, wajumbe wa pande mbili walitangaza mpango ambamo China itaagiza bidhaa za kilimo na nishati kutoka Marekani ili kupunguza nakisi ya dola bilioni 335 kila mwaka katika biashara baina ya nchi hizo.

Katika mkutano huo, Marekani ilitaka China ipunguze nakisi hiyo kwa kiasi cha dola bilioni 200 ifikapo mwaka 2020. Imearifiwa kuwa Waziri wa Biashara wa Marekani, Wilbur Ross anapanga safari ya kikazi nchini China katika muda ambao haukubainishwa.

Mazungumzo

Akihojiwa na televisheni ya Marekani Fox News, Mnuchin alisema Marekani na China zimepata maendeleo katika mazungumzo ya kiuchumi na kibiashara kati ya pande mbili yaliyomalizika hivi karibuni. Aliongeza kuwa pande hizo mbili zitaendelea na mawasiliano kuhusu masuala ya biashara.

Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki ilisema nchi hizo mbili zimeahidi kuwa hazitazusha vita vya kibiashara dhidi ya upande mwingine na zitachukua hatua madhubuti kupunguza kwa kiwango kikubwa urari wa Marekani kwenye biashara na China.