Al-Bashir awageukia polisi wake

Muktasari:

Wakati Umoja wa Mataifa (UN) ukiitisha uchunguzi dhidi ya mauaji ya waandamanaji, Rais Omar al-Bashir amelitaka Jeshi la Polisi nchini humo kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao.

Khartoum, Sudan. Wakati Umoja wa Mataifa (UN) ukiitisha uchunguzi dhidi ya mauaji ya waandamanaji, Rais Omar al-Bashir amelitaka Jeshi la Polisi nchini humo kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao.

Tangu Desemba 19, Serikali imeripoti kwamba watu 19 wamefariki dunia baada ya kukabiliana na polisi wakati wakiandamana kupinga mfumuko wa bei za bidhaa na uhaba wa mafuta nchini humo.

Wananchi hao wanapinga utawala wa al-Bashir ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1989 na kushinikiza kiongozi huyo kuachia madaraka.

Katika mkutano wake na viongozi wa juu wa jeshi la polisi jana mjini Khartoum, al-Bashir aliwaagiza kusitisha matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wakikabiliana na waandamanaji.

“Tunataka kuimarisha usalama na tunataka kufanya hivyo kwa jeshi la polisi kutumia nguvu kidogo,” alinukuliwa Rais al-Bashir na kituo cha Al Jazeera.

Nchi hiyo inakabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni na kusababisha mfumuko wa bei licha ya kuondolewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani Oktoba, mwaka jana.

Mfumuko wa bei umeongezeka kwa asilimia 70 na paundi ya Sudan imeporomoka thamani wakati uhaba wa chakula na mafuta ukiikabili miji mbalimbali nchini humo.

“Tunakubali kwamba tuna matatizo ya kiuchumi…lakini hatuwezi kuyaondoa kwa kufanya uharibifu, unyang’anyi na kuiba vitu,” alisema al-Bashir alitolea mfano baadhi ya majengo yaliyoharibiwa na waandamanaji hao.

“Hatuwezi kuruhusu nchi yetu kuwa kama nchi nyingine katika ukanda wetu zilivyokuwa. Hatutaruhusu watu wetu kuwa wakimbizi. Kama hili likitokea, tutaenda wapi katika ukanda huu?” alisema al-Bashir.