Besigye ahimiza wasomi kuacha magari yao nyumbani

Muktasari:

 

  • Ataka waonyeshe mshikamano na wananchi kuwa hawaridhishwa na mipango ya kurekebisha katiba ili kuondoa ukomo wa umri wa rais
  • Asema mgomo wa aina hii utafanyika mara moja kila wiki, hivyo badala ya kutumia magari yao wapande bodaboda na mabasi

 Mwanaharakati na kiongozi mkuu wa upinzani Dk Kizza Besigye ametoa wito kwa wasomi ambao hutumia usafiri wao kwenda kazini kushiriki mgomo wa siku moja kila wiki kupinga juhudi zinazofanywa za kuondoa ukomo wa umri wa rais.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika ofisi zake zilizoko Barabara ya Katonga jijini Kampala, Dk Besigye amewataka wasomi kuacha kutumia magari yao yenye viyoyozi mara moja kwa wiki.

"Tafadhali yaachani magari yenu nyumbani kisha mtumie usafiri wa umma. Tumieni bodaboda au mabasi au teksi … Itakuwa vizuri siku hiyo kuona magari ya umma tu, kwa vyovyote na magari ya huduma ya dharura, kama ya kubeba wagonjwa na zimamoto,” alisema Dk Besigye.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema huu ni wakati kwa wasomi kuonyesha mshikamano na raia wengine.

“Hapa inabidi wasomi waulizwe swali kama wako pamoja nasi. Kwamba nani yuko pamoja nasi ndilo swali linalofuata. Tunapendekeza kwamba siku moja katika wiki kwamba wale wasomi walioshikamana na raia wasonge mbele kwa pamoja,” aliongeza.

Huku akiwa na meya wa jiji la Kampala Erias Lukwago, Dk Besigye alimshutumu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mawasiliano Godfrey Mutabazi kwa kile alichokiita kuvikaba vyombo vya habari.

Jumatano iliyopita, baada ya askari waliokuwa wamevaa nguo za kiraia kuvamia kikao cha Bunge kilichokuwa kimegubikwa na ghasia na kuwakamata na kuwatoa nje wabunge wa upinzani Mbunge wa Jimbo la Igara Magharibi Raphael Magyezi aliruhusiwa kuwasilisha hoja yake binafsi ya kutaka yafanyike marekebisho ya Ibara ya 102 (b).

Hoja hiyo kuhusu “Mswada wa Marekebisho ya Sheria 2017” pamoja na mambo mengine inataka ifutwe Ibara ya 102 (b) katika Katiba yam waka 1995 iliyoweka ukomo wa umri wa rais kuwa miaka 75.

Wachambuzi wanaona mapendekezo hayo yamelenga kumpa nafasi nyingine Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 73 sasa kugombea urais mwaka 2021 atakapokuwa na umri wa miaka 77.