Bobi Wine ashtakiwa kwa uhaini

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi iliyotolewa Alhamisi Brigedia Richard Karemire, mbunge huyo alirejeshwa mahabusu hadi Alhamisi ijayo.

Kampala, Uganda. Mbunge wa Kyaddondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ambaye alikamatwa Jumatatu mjini Arua pamoja na wanasiasa kadhaa wa upinzani ameshtakiwa katika Mahakama ya Kijeshi mjini Gulu kwa makosa ya kukutwa na silaha na risasi kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi iliyotolewa Alhamisi Brigedia Richard Karemire, mbunge huyo alirejeshwa mahabusu hadi Alhamisi ijayo.
“Ikiwa ni sehemu ya uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu, polisi waliwakamata waandaaji wakuu na washiriki akiwemo Mheshimiwa Robert Ssentamu Kyagulanyi Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki. Katika upekuzi uliofanywa na wapelelezi kwenye chumba chake cha hoteli alikutwa akimiliki bunduki kadhaa na risasi vitu ambavyo kwa kawaida humilikiwa na Jeshi la Ulinzi,” ilisema taarifa ya Brigedia Karemire.
“Kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Kyagulanyi leo amefikishwa katika Mahakama ya Kijeshi mjini Gulu na ameshtakiwa chini ya makosa yanayoangukia S 119 (1) (h) ya Sheria ya Jeshi la UPDF, 2005 yanayohusu umiliki usiohalali wa silaha na risasi. Kisha amepelekwa mahabusu hadi Agosti 23, 2018”.
Alishtakiwa mbele ya wanasheria wake wawili; Asuman Basalirwa (Mbunge wa Manispaa ya Bugiri) na Medard Seggona (Mbunge wa Busiro Mashariki).
Kwa mujibu wa Basalirwa, ambaye alikuwepo kwenye chumba cha mahakama, uso wa mteja wake Kyagulanyi ulikuwa umevimba na hakuwa na uwezo wa kutembea wala kuongea.
Seggona alisema Kyagulanyi hakuweza hata kuandikisha maelezo kwa sababu alikuwa katika hali mbaya na amefungwa pingu.