Bobi Wine kuihudumia familia ya dereva wake

Muktasari:

  • Ametumia ziara yake hiyo kutembelea waathirika wengine walioumia kwenye vurugu zilizotokea Arua kwa madai ya kuushambulia msafara wa Rais Museveni

Kampala. Mbunge wa Kyadondo Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amesema atahakikisha anaihudumia familia ya aliyekuwa dereva wake Yasin Kawuma.

Wine alisema hayo jana akiwa nyumbani kwa dereva wake huyo aliyepigwa risasi na kupoteza maisha kwenye vurugu zilizodaiwa kutokana na kushambuliwa kwa msafara wa Rais Yoweri Museveni.

Dereva huyo alirushiwa risasi na watu wanaodaiwa walikuwa walinzi wa Rais Museveni wakati akimwendesha Bobi Wine eneo la Arua.

Baada ya kukutana na mjane wa dereva huyo eneo la Kiteezi wilayani Wakiso, Wine alisema yuko tayari kuihudumia familia hiyo mpaka dakika za mwisho za maisha yake.

"Najua familia hii kwa sasa ipo kwenye wakati mgumu nitaisadia kwa jinsi nitakavyoweza, lakini ngoja tuendelee na mapambano,’’alisema.

Pia familia hiyo ilimshukuru mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki kwa ujio wake huo na kutoa ahadi ya kuisadia.

Pia mbunge huyo aliwatembelea watu wengine waliokuwa wamelazwa hospitali mbalilimbali wakipatiwa matibabu kutokana na shambulio hilo.