Bunge kuchunguza ukatili wa jeshi kwa wananchi

Muktasari:

  • Ni wa kikosi cha kuzuia uvuvi haramu wanaodaiwa kupiga wananchi wa jamii ya wavuvi

Kampala, Uganda. Maofisa wa Kikosi cha Kulinda Uvuvi, ambacho ni sehemu ya brigedi ya Jeshi la Majini (UPDF), wako chini ya uchunguzi kutokana na ukatili wanaodaiwa kuwafanyia wananchi wa jumuiya ya wavuvi.
Naibu Spika wa Bunge, Jacob Oulanyah ameagiza Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo kuchunguza suala hilo na kuwasilisha haraka ripoti yake bungeni.
“Tunataka kupata ufumbuzi; hivyo naiagiza kamati kuchunguza na kuja na ripoti kamilifu,” alisema Oulanyah.
Naibu spika alisisitiza kwamba suala hilo lazima lifanyiwe kazi haraka kwa vile linahusisha maisha ya watu.
Maagizo ya spika yamekuja baada ya mjadala uliorefushwa na wabunge.