Chameleon amwangukia Rais Museveni amsamehe Bobi Wine

Muktasari:

  • Wakati Polisi wakieleza hivyo, ndugu zake wanasema hadi sasa hawajui alipo.

Uganda.  Mwanamuziki Jose Chameleon amemuombea msamaha kwa Rais Yoweri Museven msanii mwenzake Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, anayedaiwa kushikiliwana jeshi la polisi nchini humo.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya dereva wa mwanamuziki huyo ambaye pia ni mbunge wa  Kyadondo Mashariki, kuuawa kwa kupigwa risasi.

Tukio hilo  lilitokea katika vurugu za kampeni za ubunge zinazoendelea nchini humo ambapo Bobi anaelezwa kumuunga mkono mgombea huru.

Baada ya tukio hilo, Bobi inadaiwa kuwa anashikiliwa kwa tuhuma za uchochezi, japokuwa polisi wanadai kwamba yupo katika matibabu.

Wakati Polisi wakieleza hivyo, ndugu zake wanasema hadi sasa hawajui alipo.

Katika barua yake aliyoandika kwenda kwa Rais Museveni,  Chameleon, amesema ameamua kuweka pembeni tofauti zake na Bobi na kumuombea msamaha.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa  Instagram, mwanamuziki huyo amekiri kuwa pamoja na kwamba Bobi katika tukio hilo amefanya kosa ni vyema Museveni kuwa mfano wa kusamehe kwenye Taifa hilo kwa kuwa hakuna kosa lisilosameheka.