Dunia yapongeza Korea mbili kujadili amani yao

Muktasari:

Brussels, Ubelgiji. Viongozi mbalimbali wa kimataifa wamepongeza mkutano wa kihistoria kati ya viongozi wa Korea ya Kaskazini na Kusini uliofanyika Ijumaa wakisema ni hatua ya kuelekea amani, lakini pia walitoa tahadhari kuhusu changamoto zilizo mbele yao.

Wafurahishwa na hatua ya viongozi wa nchi jirani kukutana na kuzungumzia amani yao lakini wametahadharisha ugumu wa kazi iliyo mbele yao

Brussels, Ubelgiji. Viongozi mbalimbali wa kimataifa wamepongeza mkutano wa kihistoria kati ya viongozi wa Korea ya Kaskazini na Kusini uliofanyika Ijumaa wakisema ni hatua ya kuelekea amani, lakini pia walitoa tahadhari kuhusu changamoto zilizo mbele yao.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In, katika mkutano wao wa kwanza baada ya miaka 11, walikubaliana kufuata njia ya amani pamoja na makubaliano ya kudumu na kuachana na silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.

Wakati tu utasema

“Baada ya mwaka wa hasira ya uzinduzi wa silaha na majaribio ya nyuklia, mkutano wa kihistoria kati ya Kaskazini na Korea ya Kusini sasa unafanyika,” alisema Rais wa Marekani Donald Trump kwa njia ya Twitter.

“Mambo mazuri yanatokea, lakini muda tu utasema!” aliongeza Trump, ambaye anatarajia kukutana na Kim wiki chache zijazo.

Katika ‘twiti’ ya pili, Trump aliandika: “Kumalizika vita vya Korea! Marekani, na watu wake wote mashuhuri, wanapaswa kufurahia kwa kinachofanyika Korea sasa!”

Safari mpya ya utulivu

“Tunashukuru hatua ya kihistoria ya viongozi wa Korea na tunathamini maamuzi yao kisiasa na ujasiri,” msemaji wa mambo ya nje wa China, Hua Chunying aliwaambia waandishi wa habari.

“Tunatumaini na tunawatarajia watatumia fursa hii kufungua safari mpya ya utulivu wa muda mrefu kwenye eneo hilo la rasi,” alisema mwanamama huyo. Pia, alinukuu shairi ambalo linasomeka: “Tunabaki ndugu baada ya mabadiliko yote, hebu tuache kinyongo cha zamani, tutabasamu tunapokutana tena.”

Kuangalia harakati za Kaskazini

“Leo Rais Moon Jae-in na Mwenyekiti Kim Jong Un walifanya majadiliano kwa bidii kuhusu Korea Kaskazini kuondokana na silaha za nyuklia. Napenda kukaribisha uamuzi huo kuwa ni hatua nzuri kuelekea azimio kamili la masuala mbalimbali kuhusu Korea ya Kaskazini,” Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe aliwaambia waandishi wa habari. “Tunatarajia Korea ya Kaskazini itachukua hatua thabiti kupitia mkutano huu na mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

“Tutaendelea kuangalia mustakbali wa baadaye wa Korea Kaskazini. Kwa vyovyote vile, natamani kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya Japan, Marekani na Korea Kusini kuelekea ufumbuzi kamili wa masuala ya kuteketezwa, nyuklia na makombora na kuelekea mazungumzo ya Marekani-Kaskazini ya Korea.”

Habari njema

“Hii ni habari nzuri sana,” Dmitry Peskov msemaji Rais wa Urusi Vladimir Putin aliwaambia waandishi wa habari.

“Leo tunaona kuwa majadiliano haya ya moja kwa moja yamefanyika (na) yana matarajio fulani. Shauku ya kutafuta makubaliano yanaweza kuonekana kwa pande zote mbili, likiwemo jambo muhimu sana – nia njema ya kuanza na kuendeleza mazungumzo. Huo ni ukweli bayana,” alisema.

Kazi ngumu mbele

“Hii ni hatua ya kwanza ambayo inatia moyo, lakini tunatakiwa kutambua kwamba bado kuna kazi nyingi ngumu zilizo mbele yetu,” mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema kwa makini katika mkutano wa mawaziri wa kigeni wa NATO huko Brussels, Ubelgiji.

Dhidi ya tabia zote

Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini alisema kwamba “mkutano unaonyesha kwamba njia ya amani inawezekana, dhidi ya tabia zote.”

Alisema kwamba EU ilikuwa tayari kutoa “msaada kamili kwa kufikia kuondokana na silaha za nyuklia katika rasi.”

“Umoja wa Ulaya, leo kama kawaida yake, unasimama upande wa amani, upande wa kuachana na silaha za nyuklia na kwa ustawi wa baadaye kwa Wakorea wote,” alisema mwanamama huyo katika taarifa yake.

Maswali mengi yamebaki

“Nimefurahishwa sana na kile kilichotokea. Sidhani kuwa mtu yeyote anayeangalia historia ya Korea Kaskazini ya mipango ya kuendeleza silaha ya nyuklia atakuwa na matumaini makubwa sana lakini ni habari njema nzuri kwamba wawili wamekutana,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Boris Johnson alisema mjini Brussels.

“Mkutano huu wa kihistoria si mwisho kwao. Bado kuna maswali mengi yanayopaswa kujibiwa,” aliongeza katika taarifa.