ICC yaitunishia kifua Marekani

Muktasari:

  • Yasema itaendelea kutimiza wajibu wake bila kutishwa na taifa hilo kubwa lenye nguvu za kiuchumi na kijeshi

The Hague, Uholanzi.  Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imesema itaendelea na kazi zake bila kuogopa baada ya Marekani kutishia kuwashtaki majaji na maofisa wake endapo raia yeyote wa Marekani atashtakiwa kwa uhalifu wa kivita alioutenda nchini Afghanistan.
Ufaransa na Ujerumani zimelitia uzito kuiunga mkono Mahakama hiyo yenye makao yake Hague baada ya mshauri wa masuala ya usalama kitaifa nchini Marekani, John Bolton kusema: "Mahakama ya ICC tayari imekufa kwetu sisi."
Taarifa iliyotolewa jana na Mahakama hiyo kufuatia kitisho hicho cha Marekani ilisema, ICC kama Mahakama ya sheria itaendelea kutimiza wajibu wake bila kuogopeshwa, kwa kuzingatia misingi na wazo mtambuka la utawala wa kisheria.
Katika kuonyesha uungwaji mkono, chombo hicho cha kusimamia sheria kilisema kinapata ushirikiano madhubuti na kuungwa mkono na nchi wanachama 123 pamoja na mataifa mengine na mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia.
Mataifa muhimu yenye nguvu yaliitetea Mahakama ya ICC iliyoanzishwa mwaka 2002 ikiwa na mamlaka ya kuchunguza na kushtaki waliotenda uhalifu mbaya kabisa dunia yakiwamo mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
"Ufaransa na washirika wake wa Ulaya inaunga mkono ICC kifedha na ushirikiano. Mahakama lazima iwe na uwezo wa kuchukua hatua na kutumia mamlaka yake bila kuzuiwa kwa uhuru na kuzingatia maadili,",” ilisema wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa.