Kabila apanga kugombea urais 2023

Muktasari:

  • Kauli kwamba Kabila atasalia katika siasa imemwibua Katibu wa chama cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC), Eve Bazaiba, ambaye amesema kimsingi ndiye atakuwa anaongoza na siyo mgombea urais kupitia muungano wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary ikiwa atashinda

Kinshasa, DR Congo. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Joseph Kabila Jumapili alisema anapanga kuendelea kushiriki siasa hata baada ya kung’atuka madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wa Desemba 23.
Katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, Kabila alisema pia hafuti uwezekano wa kugombea tena urais mwaka 2023.
Kuhusu jukumu lake baada ya uchaguzi huo, ambao yeye hatagombea, alisema atasaidia kuhakikisha taifa linabaki imara.
“Jukumu langu litakuwa kuhakikisha kwamba haturudi tena nyuma tulikotoka. Yaani kule tulikoikuta Congo miaka 20 au 22 iliyopita. Wajibu wangu utakuwa kutoa ushauri, kwa kuwapa taarifa zote muhimu, ushauri wa kuchukua au kutochukua ili kwamba tusirudi tena kwenye miaka ile ambayo inapaswa kubaki kuwa historia,” alisema Kabila aliyetarajiwa kuondoka madarakani miaka miwili iliyopita baada ya kuongoza kwa mihula miwili kwa mujibu wa katiba.
Kauli kwamba Kabila atasalia katika siasa imemwibua Katibu wa chama cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC), Eve Bazaiba, ambaye amesema kimsingi ndiye atakuwa anaongoza na siyo mgombea urais kupitia muungano wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary ikiwa atashinda.
"Anataka tu kusalia madarakani. Hata kama alimchangua Shadary, Shadary ni mtu tu wa kuonekana, ndiye atakayemuongoza Shadary kwa kila jambo. Kiuhalisia, atakuwa bado ndiye rais."
Uchaguzi wa mwaka huu ambao umecheleweshwa sana utakuwa wa kwanza DRC wa kubadilishana mamlaka kidemokrasia na kuhitimisha utawala wa Kabila aliyetawala tangu mwaka 2001 baada ya kifo cha baba yale Laurent Desire Kabila.
Pia alisema kuwa imewachukua muda mrefu kuandaa uchaguzi huo kwa sababu wanataka ufanyike vizuri.
Agosti, mwaka huu Kabila alimtangaza mshirika wake wa karibu, Emmanuel Ramazani Shadary ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani kuwa mgombea wa muungano wa kisiasa unaotawala kwa sasa.
Shadary amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kutokana na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.