Kabila azusha furaha, sintofahamu DRC

Muktasari:

  • Lakini wasiwasi utaendelea kuwepo kwamba Kabila, kwa kumteua mgombea mtiifu kwake aweze kugombea katika uchaguzi mkuu wa Desemba 23, analenga kutumia ushawishi wa kiti hicho cha enzi, wachambuzi wanasema.

Kinshasa, DR Congo. Kwa kutangaza kuwa anajiweka kando baada ya kutawala kwa miaka 17 Rais Joseph Kabila amepunguza hofu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo lakini nchi bado inakabiliwa na sintofahamu kuelekea uchaguzi uliopangwa Desemba 23.
Mashinikizo kutoka ndani ya nchi, kanda na kimataifa yanaweza kuwa yamechangia uamuzi wa Rais uliokuwa unasubiriwa sana wa kumteua mrithi badala ya kujitaja yeye mwenyewe.
Lakini wasiwasi utaendelea kuwepo kwamba Kabila, kwa kumteua mgombea mtiifu kwake aweze kugombea katika uchaguzi mkuu wa Desemba 23, analenga kutumia ushawishi wa kiti hicho cha enzi, wachambuzi wanasema.
"Kabila amekwepa swali juu ya malengo yake kutoka kwenye ajenda kwa kumchagua mrithi," alisema Hans Hoebeke, mchambuzi mkuu wa Congo kutoka Taasisi ya Kimataita ya Utatuzi Migogoro (ICG), alipohojiwa na shirika la habari la AFP.
"Hali hii isiwape watu uhakika mkubwa. Hakuna hakikisho kwamba uchaguzi utafanyika kwa yakini, na ukifanyika, kwamba utaweza kufikia walau kigezo cha chini cha kuaminika."
Kabila ametawala tangu mwaka 2001 alipouawa baba yake, Laurent-Desire. Utawala wake uligubikwa na matukio ya  migogoro na ufisadi.
Baada ya mihula yake miwili kumalizika mwaka 2016, Kabila aliendelea kubaki mamlakani akaingiza katika katiba ibara ya kuongoza kipindi cha mpito ili aendelee mamlakani. Katika miezi ya hivi karibuni, aliwaacha watu wawe wanakisia kuhusu hatima yake.
Jumatano, saa kadhaa kabla ya muda wa mwisho wa kujaza fomu za kugombea urais kupitia chama chake cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), ofisi yake ikatoa tangazo muhimu.
Hapo ndipo Kabila alimtangaza waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mgombea urais kupitia chama tawala cha PPRD.
Kwa kumchagua mshirika wake tena ambaye amewekewa vikwazo na nchi za Ulaya kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, Kabila ameonyesha ishara kwamba utiifu unazingatiwa juu ya mambo mengine yote.
Shadary atapambana dhidi ya orodha ndefu ya wagombea wa upinzani na hana umaarufu mkubwa nchini.
"Ngome yake ya kisiasa iko Maniema, jimbo dogo mashuhuri kwa uchimbaji madini ambalo linajumuisha chini ya asilimia tano ya majimbo ya uchaguzi DRC,” alisema Indigo Ellis mchambuzi wa majanga kutoka kampuni ya Verisk Maplecroft.