Kagera waanzisha madawati upimaji Ebola mipakani

Muktasari:

  • Hatua hiyo imechukulia baada ya kuibuka kwa ugonjwa huo DRC.

 Mkoa wa Kagera umechukua tahadhari ya ugonjwa wa Ebola ulioibuka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kwa kuanzisha madawati ya afya katika maeneo yote ya mipakani kwa ajili ya kuwapima wanaoingia Tanzania kutokea nchini humo.

Akizungumza na MCL Digital Kaimu Ofisa Afya mkoa wa Kagera, Gerazi Ishengoma amesema hatua hiyo imechukuliwa tangu Aprili 8, 2018 ugonjwa wa Ebola uliporipotiwa kuibuka Congo.

Ametaja vituo vya mipakani vilikofunguliwa kuwa ni Mtukula wilaya ya Misenyi, Murongo wilaya ya Kyerwa, Kabanga na Rusumo wilayani Ngara.

Kwa mujibu wa Ishengoma, miongoni mwa dalili za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, uchovu, maumivu ya koo, tumbo, misuli, kuumwa kichwa na viungo vingine, kichefuchefu na kuhara pamoja na figo kutofanya kazi vizuri.

Mtu anayeugua ugonjwa huo pia hutokwa na damu sehemu zote za wazi za mwili kuanzia kwenye vinyweleo, pua, mdomoni na masikio, dalili zinazoonekana kati ya siku mbili hadi wiki tatu baada ya kuambukizwa.

Inapofikia hatua ya juu, mgonjwa wa Ebola hupata mshtuko wa moyo, shinikizo la damu, mapigo ya moyo kwenda kasi, kupungua kwa mzunguko wa damu mwilini,maumivu ya viungo na hatimaye viungo kushindwa kufanya kazi.