Kampeni uchaguzi mkuu DRC kuanza Alhamisi

Muktasari:

  • Wakati kila chama cha upinzani kinatarajiwa kuingia kivyake katika uchaguzi huo, muungano wa vyama tawala FCC umejipanga kwa mikutano ya kuwaandaa watu 500 watakaozunguka nchi nzima kumtafutia kura mgombea wao Shadary.

Kinshasa, DR Congo. Kampeni za uchaguzi mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) uliopangwa kufanyika Desemba 13, zinatarajiwa kuanza keshokutwa Alhamisi huku upinzani ukiwa umeshindwa kukubaliana kuwa na mgombea mmoja.
Katika mkutano wao uliofanyika Geneva, Uswisi ukishirikisha vyama vikuu vya upinzani Novemba 11, wajumbe waliafikiana mwanasiasa Martin Fayulu apeperushe bendera ya upinzani, lakini uteuzi wake ulipingwa na wafuasi wa vyama vikubwa vya UDPS kinachoongozwa na Felix Tshisekedi, na UNC cha Vital Kamerhe. Wanasiasa wawili hao walijiondoa katika makubaliano.
Juhudi za Fayulu kuwasihi Tshisekedi na Kamerhe kubaki katika umoja huo zilikwama na sasa wote wanatarajiwa kurejea nyumbani wiki hii kwa ajili ya kampeni kali kukabiliana na mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.
Fayulu, mbunge asiyefahamika sana DR Congo aliwasihi wanasiasa waliojiondoa kufikiria upya. "Makubaliano bado hai," alisema Fayulu kupitia televisheni ya TV5Monde kuhusu mtafaruku huo.
"Nawahimiza kaka zangu warejee tufikirie na tutoe kipaumbele kwa maslahi mapana ya taifa letu,” alisema kwa twitter. "Bado hatujachelewa kufanya jambo sahihi."
Wakati kila chama cha upinzani kinatarajiwa kuingia kivyake katika uchaguzi huo wa kwanza bila jina la Rais Joseph Kabila kuwepo kwenye karatasi za kupigia kura, muungano wa vyama tawala FCC umejipanga kwa mikutano ya kuwaandaa watu 500 watakaozunguka nchi nzima kumtafutia kura mgombea wao Shadary.