Magazeti Marekani yaungana kumkosoa Trump

Muktasari:

  • Magazeti zaidi ya 350 yaliitikia wito wa gazeti la Boston Globe kuandika katika safu zao za tahariri Alhamisi kupigania “uhuru wa habari kutokana na mashambulizi ya Rais Trump

Washington, Marekani. Mamia ya magazeti nchini Marekani yameandika maoni ya mhariri yakishutumu tabia ya Rais Donald Trump kuvishambulia vyombo vya habari, zikiwa ni juhudi za pamoja na kuunganisha nguvu kukuza uhuru wa habari.
Magazeti zaidi ya 350 yaliitikia wito wa gazeti la Boston Globe kuandika katika safu zao za tahariri Alhamisi kupigania “uhuru wa habari kutokana na mashambulizi ya Rais Trump mara kwa mara dhidi ya vyombo vya habari".
Trump amekuwa akivikosoa vyombo vya habari kwenye hotuba zake kwa umma na kupitia akaunti yake ya Twitter, akivielezea kuwa vinatoa habari za upotoshaji na adui kwa umma.
"Waandishi wa habari si maadui," kilisomeka kichwa cha tahariri katika gazeti la Boston Globe Alhamisi.
Maoni hayo yalisema kuwa "uongo ni kinyume cha maadili kwa raia wenye ufahamu, wanaowajibika na wanaopendelea uongozi wa kujitawala." Yaliendelea kusema, "Ubora wa Marekani unategemea jukumu la uhuru wa vyombo vya habari kusema ukweli dhidi ya wenye nguvu."
Maoni hayo yalihitimisha kwa kusema "kuviita vyombo vya habari kuwa ni adui wa watu" ni kinyume na Marekani kwani ni hatari kwa umoja wa raia tunaoushiriki kwa pamoja kwa karne mbili."
Gazeti la New York Times katika tahariri yake liliandika: "Kuvishutumu vyombo vya habari - kwa kupinga au kupindua habari ili kuwa na uelewa potofu - unaona sawa...Lakini kusisitiza kwamba ukweli usioupenda ni ‘habari bandia’ ni hatari kwa maisha ya demokrasia. Na kuwaita wanahabari ‘adui wa watu’ ni hatari, kipindi.”
Tangu alipoingia madarakani mwaka jana, Trump amekuwa akivishutumu vyombo vya habari mara kwa mara, mara nyingine akitaja baadhi ya magazeti kuwa “habari bandia”.