Majanga zaidi yamfuata Robert Mugabe

Muktasari:

  • Msemaji wa Chama cha Taifa cha Maveterani wa Vita vya Ukombozi Douglas Mahiya amethibitisha maendeleo hayo mapya akiwa na viongozi wa chama cha MDC-T na wale wa Zimbabwe Economic Freedom Fighters (EFF) wakisema wako pamoja katika kampeni ya kumpokonya Mugabe mashamba 20 na kumwachia moja kama inavyosema sera ya Serikali mtu mmoja shamba moja.

Harare, Zimbabwe. Miaka michache iliyopita rais wa zamani Robert Mugabe aliwaongoza maveterani wa vita kuvamia mashamba ya walowezi na kupora na kujimilikisha, lakini miezi michache tangu alipoondolewa madarakani mkongwe huyo amegeukwa. Sasa maveterani walewale, katika mazingira nadra kuonyesha mshikamano, wameungana na vyama vya upinzani kufanya kampeni mpya ya kumpokonya Mugabe mashamba kadhaa anayomiliki ili yagawanywe upya kwa mamilioni ya Wazimbabwe wanye uhitaji.

Msemaji wa Chama cha Taifa cha Maveterani wa Vita vya Ukombozi Douglas Mahiya amethibitisha maendeleo hayo mapya akiwa na viongozi wa chama cha MDC-T na wale wa Zimbabwe Economic Freedom Fighters (EFF) wakisema wako pamoja katika kampeni ya kumpokonya Mugabe mashamba 20 na kumwachia moja kama inavyosema sera ya Serikali mtu mmoja shamba moja.

“Tulimpinga Mugabe kwa sababu ya ufisadi wake na tumesema kwa muda mrefu kwamba sera ya mtu mmoja shamba moja lazima itekelezwe bila upendeleo. Katika hili hatumuungi mkono wala hatumlengi Mugabe kwa masuala binafsi, lakini huu umekuwa wito wetu kwa sauti za juu kwamba ufisadi wa Mugabe unanuka Zimbabwe kote kuanzia mashamba lukuki anayomiliki,” alisema Mahiya.

Mugabe kwa hakika amewekwa chini ya mzingiro na watendaji wakuu wa chama tawala cha Zanu PF tangu alipong’olewa madarakani Novemba mwaka jana katikati ya ripoti kwamba mashamba ya Mazowe, ambako mkewe Grace Mugabe alijenga nyumba kwa ajili ya kulea yatima na ameotesha miti ya matunda ya malimau na shamba la ng’ombe wa maziwa limevamiwa na wachimbaji wa dhahabu.

Katibu mkuu wa MDC-T, Douglas Mwonzora alisema kampeni hiyo wala haimlengi Mugabe pekee bali wamiliki wote wenye mashamba mengi.

“Kuna viongozi wengine waandamizi katika Zanu PF na serikali ambao wanamiliki pia mashamba mengi. Litakuwa jambo baya kumlenga mtu mmoja au familia moja. Watu wote wanaomiliki mashamba mengi wahimizwe kurejesha.”

ili wapewe raia wengine wa Zimbabwe wasio na ardhi,” alisema.