Makanisa yatishiwa kufungwa Mbale

Muktasari:

  • Naibu meya wa jiji, Kenneth Waniaye Khatuli alisema kwamba amepokea malalamiko mengi kutoka kwa watu wanaoishi jirani na makanisa hayo kwamba yanapiga kelele mno wakati wa ibada zao usiku.

Mbale, Uganda. Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mbale wametishia kufunga makanisa ya waumini wa Kikristo maarufu kama walokole kwa kupiga kelele kupita kiasi hali sawa na uchafuzi wa sauti.
Naibu meya wa jiji, Kenneth Waniaye Khatuli alisema kwamba amepokea malalamiko mengi kutoka kwa watu wanaoishi jirani na makanisa hayo kwamba yanapiga kelele mno wakati wa ibada zao usiku.
“Tutaanza kufunga moja baada ya jingine na operesheni hii itaendelea hadi tuhakikishe hakuna kelele mjini na viunga vya mji. Makanisa hayo lazima yapige muziki kwa viwango vya chini,” alisema.
Kwa mujibu wa Khatuli, watu wanaoishi jirani na makanisa ya walokole wanashindwa kulala usiku kwa sababu ya kelele zinazotoka kwenye maeneo ya ibada.
“Maeneo hayo yanaleta usumbufu kwa amani ya umma kutokana na kelele zinazotoka kwenye spika zao,” alisema.