Saudi Arabia yataka waliomuua Khashoggi wauawe

Muktasari:

  • Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi mjini Riyadh, naibu mwendesha mashtaka mkuu wa umma Shaalan al-Shaalan, alisema "kisa hicho" kilianza Septemba 29




Riyadh, Saudi Arabia. Sakata la kuuawa kwa mwanahabari Jamal Khashoggi limechukua sura mpya baada ya ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa umma kupendekeza hukumu ya kifo dhidi ya washukiwa watano kati ya 11 waliokuwa wameshtakiwa.
Uamuzi huo ulitolewa Alhamisi na naibu mwendesha mashtaka mkuu wa umma, Shaalan al-Shaalan aliyetoa matokeo ya uchunguzi wake ambao ulionyesha dhahiri mwanamfalme Mohammed bin Salman (MBS) hakuhusika.
Katika uchunguzi huo, Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu imesema aliyeamuru kuuawa kwa Khashoggi ni ofisa mwandamizi wa idara ya usalama wa taifa ya Saudia ambaye alipewa kazi ya kumshawishi mwanahabari huyo kurejea Saudia.
Hata hivyo, matokeo hayo yamepuuzwa na maofisa wa Uturuki ambao wamedai hautoshi huku Marekani ikiamua kuwawekea vikwazo maofisa 17 wa Saudi Arabia ambao imedai walihusika na mauaji hayo.
Msimamo wa maofisa wa Uturuki ni kwamba hakukuwa na uwezekano kwa Khashoggi kuuawa bila MBS kujua, na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema amri ilitolewa na “mamlaka za juu katika Serikali ya Saudi Arabia."
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, ofisa mmoja katika kikosi kilichomuua Khashoggi alipiga simu punde akimwambia ofisa mwingine Saudi Arabia "mjulishe bosi wako" kwamba mauaji yametekelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi mjini Riyadh, naibu mwendesha mashtaka mkuu wa umma Shaalan al-Shaalan, alisema "kisa hicho" kilianza Septemba 29 wakati “aliyekuwa” naibu mkuu wa usalama wa taifa alipoamuru “kiongozi wa mpango” huo “kumrejesha nyumbani mtuhumiwa kwa mbinu zozote za ushawishi, na ikiwa ushawishi utashindikana, basi zitumike nguvu”.
Japokuwa ofisi ya mwendesha mashtaka haikutaja majina ya wahusika, Jenerali Ahmad al-Assiri, ambaye alifutwa kazi kama mkuu wa intelijensia siku ya mkesha wa mauaji hayo, anadaiwa kuwa mmoja wa watu wa kuuawa.
Kiongozi wa msafara, ambaye pia hakutajwa, aliiweka timu nzima ya watu 15 jukumu la “kumrejesha” mwandishi huyo kutoka Uturuki.
Mwanahabari huyo ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa bin Salman alikimbia Saudia mwaka 2017 na kuhamia Marekani.
Msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu, alisema Khashoggi alidungwa sindano ya sumu baada ya kuibuka tafrani ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul, Oktoba 2, 2018.