Marekani yaomba mkanda wa mauaji ya mwandishi wa Saudi Arabia

Muktasari:

  • Trump amesema anatarajia ripoti kutoka kwa waziri wake wa Mambo ya Nje Mike Pompeo ambaye alikua nchini Saudi Arabia na Uturuki.

Washington, Marekani. Serikali ya Marekani imeiomba Uturuki kutoa ushahidi wa kanda ya sauti inayodai kuwa mwandishi Jamal Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

Rais wa Marekani, Donald Trump amewaambia waandishi katika Ikulu ya White House kuwa, "Tumeomba kupewa nakala ya kanda hiyo, kama kweli ipo."

Khashoggi hajawahi kuonekana tangu alipoingia jengo la ubalozi wa Saudi Arabia Oktoba 2 mwaka huu. Saudi Arabia imekanusha kuhusika na mauaji hayo.

Wakati hayo yakijiri, Gazeti la Washington Post limechapisha makala za mwisho zilizoandikwa na mwandishi huyo kabla ya kutoweka kwake.

Katika makala hizo anazungumzia umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mhariri wa kimataifa wa gazeti hilo, Karen Attiah amesema uchapishaji wa makala hizo ulisitishwa kwa sababu walikuwa na matumaini kwamba Khashoggi angerejea salama.

Ameandika akisema: "Sasa sina budi kukubali kwamba hilo halitafanyika.” Hii ndio makala yake ya mwisho nitakayosahihisha".

Attiah amesema: "Makala hiyo inaangazia kwa kina kujitolea kwake kupigania uhuru katika mataifa. Uhuru ambao alipigania kwa maisha yake."

Ripoti katika vyombo vya habari vya taifa hilo zinaelezea taarifa za kutisha za dakika za mwisho za mwandishi huyo.

Gazeti moja la Uturuki linasema sauti ya balozi wa Saudi Arabia mwenyewe Mohammed al Otaibi inasikika katika kanda hiyo iliyonasa kifo cha Khashoggi.

Redio Yeni Safak ambayo ina uhusiano wa karibu na Serikali imemnukuu balozi huyo akidai kuwa Saudia ilituma maajenti mjini Istanbul: "Msiseme hili, mtanitia matatani."

Akigusia sauti iliyorekodiwa na ambayo inadaiwa kuwa na ushahidi wa mauaji ya Khashoggi ,Trump aliongeza: "Sina uhakika ya kuwepo kwa sauti hiyo, lakini huenda ikawa ni kweli ipo."