Uchunguzi mauaji ya rais wa zamani Rwanda wasitishwa

Rais wa  zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana

Muktasari:

  • Kifo cha Habyarimana kilichochea mauaji ya kimbari ambapo wapiganaji wenye msimamo mkali wa Kihutu waliwauwa Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani zaidi ya 800,000.

Kigali, Rwanda. Mwendesha mashtaka nchini Ufaransa amependekeza kutupiliwa mbali tuhuma zinazowakabili maofisa wanane wa ngazi ya juu wa Rwanda akiwemo Waziri wa Ulinzi waliokuwa wakichunguzwa kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana kilichotokea mwaka 1994.
Uchunguzi huo ulioanzishwa Ufaransa mwaka 1998 baada ya ndugu wa raia wa Ufaransa waliofariki dunia kwenye ndege iliyokuwa imembeba Habyarimana ilipotunguliwa kusababisha mvutano mkubwa kati ya Ufaransa na Rwanda kwa miongo zaidi ya miwili.
Kutokana na uamuzi huo wa mwendesha mashtaka sasa ni juu ya mahakimu wanaohusika na uchunguzi kuamua kusitisha mchakato wa uchunguzi au kuendelea na kupeleka kwenye baraza la mahakama.
Kifo cha Habyarimana kilichochea mauaji ya kimbari ambapo wapiganaji wenye msimamo mkali wa Kihutu waliwauwa Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani zaidi ya 800,000.
James Kabarebe Waziri wa Ulinzi wa Rwanda ni mmoja wa maofisa waliokuwa wakilengwa katika uchunguzi huo.