May aapa kuendeleza mchakato wa Brexit

Muktasari:

  • Kiongozi huyo wa chama cha Conservative alisema kuukataa mkataba wa Brexit kutaiweka nchi katika “njia mbaya na mashaka makubwa” na akaweka wazi kuwa kamwe haitafanyika kura ya maoni nyingine.
  • Hadi alipokuwa zkizungumza na waandishi wa habari, May alikuwa amepata pigo baada ya mawaziri wanne kujiuzulu nyadhifa zao siku moja baada ya waziri mkuu huyo kutangaza kuwa baraza lake la mawaziri lilikuwa limeridhia rasimu ya makubaliano ya Brexit.
  • Katika kura ya maoni iliyoendeshwa Juni 2016, asilimia 52 ya Waingereza iliamua kujiondoa EU, huku asilimia 48 ikitaka kubaki.

London, Uingereza. Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameapa kusonga mbele na kufanikisha mpango wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) licha ya mawaziri wake kujiuzulu mfululizo na mnyukano ndani ya chama unaoweka shakani uwaziri mkuu.
Katika mkutano wa waandishi wa habari aliouitisha Alhamisi kwenye makazi yake, May akionyesha ujasiri alisisitiza kuwa mkataba uliopendekezwa juu ya Uingereza kuachana na umoja huo kwanza umeweka mbele “maslahi ya taifa” na ndiyo njia ya kukwepa kutokuwepo mkataba wa mchakato huo maarufu kama Brexit.
Kiongozi huyo wa chama cha Conservative alisema kuukataa mkataba wa Brexit kutaiweka nchi katika “njia mbaya na mashaka makubwa” na akaweka wazi kuwa kamwe haitafanyika kura ya maoni nyingine.
Hadi alipokuwa zkizungumza na waandishi wa habari, May alikuwa amepata pigo baada ya mawaziri wanne kujiuzulu nyadhifa zao siku moja baada ya waziri mkuu huyo kutangaza kuwa baraza lake la mawaziri lilikuwa limeridhia rasimu ya makubaliano ya Brexit.
Katika kura ya maoni iliyoendeshwa Juni 2016, asilimia 52 ya Waingereza iliamua kujiondoa EU, huku asilimia 48 ikitaka kubaki.