Friday, August 12, 2016

Mchuano mkali urais Zambia

 

Lusaka, Zambia. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zambia imeanza kuhesabu kura kufuatia uchaguzi wa wabunge na urais huku kukitarajiwa kuwepo mchuano mkali baina ya Rais Edgar Lungu na mfanyabiashara tajiri Hakainde Hichilema.

Mamia ya wananchi wamejitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura licha ya kuwepo hali ya wasiwasi kutokana na ghasia zilizozuka wakati wa kampeni.

Lungu anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama tawala  cha Patriotic Front (PF) huku mpinzani wake mkuu Hichilema akisimamia kuwania urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha United Party for National Development (UPND).

Lungu alimshinda kwa taabu mfanyabiashara huyo tajiri katika uchaguzi mdogo wa rais wa mwaka jana ulioitishwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Michael Sata ambaye alifariki dunia Oktoba 28, 2014. Wasiwasi umetanda katika baadhi ya miji kutokana na kampeni za uchaguzi huo kumalizika kwa vurugu na machafuko.

Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, uchaguzi huo utaingia duru ya pili kutokana na kuwa, hakuna mgombea yeyote wa kiti cha urais atakayeweza kujipatia zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Jumuiya za kimataifa zimetuma waangalizi wake katika uchaguzi huo unaotajwa kuwa ni kipimo cha ukomavu wa demokrasia katika taifa hilo maarufu wa uchimbaji wa madini ya shaba. Kuporomoka kwa bei ya shaba nyekundi kumesababisha kufungwa kwa migodi na maelfu ya watu wakipoteza kazi.

-->