Mgombea aahidi kubadili jina la Zimbabwe

Muktasari:

  • Zikiwa zimebaki siku chache kufanyika uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe, kiongozi wa MDC-T ameapa kubadili jina la nchi hiyo.

Si mara ya kwanza kwa nchi hiyo kubadili jina na hata baadhi ya nchi za Afrika nazo pia zimebadili majina yake kwa sababu mbalimbali

Harare, Zimbabwe. Zikiwa zimebaki siku chache kufanyika uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe, kiongozi wa MDC-T ameapa kubadili jina la nchi hiyo.

Kiongozi huyo, Nelson Chamisa ameapa kuwa atalibadilisha jina la nchi hiyo na kuwa ‘Great Zimbabwe’ akieleza kuwa lile la sasa la nchi hiyo lina laana.

“Zimbabwe haiwezi kuendelea kuwa Zimbabwe kwa sababu imegeuzwa kuwa gofu la Zimbabwe,” Chamisa aliwaambia maelfu ya wafuasi wake katika mkutano wa hadhara mashariki mwa mji wa Mutare.

“Jina la Zimbabwe limelaaniwa kama mnavyoona timu yetu ya Taifa ya soka inashindwa kila mashindano, hata mchezo wa kriketi tunashindwa.”

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 40 ana lengo la kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa kwanza utakaofanyika Julai 30 tangu alipoondoka madarakani Robert Mugabe.

Kwa mujibu wa Shirika Utangazaji la Uingereza (BBC), suala la kubadili jina kwa Zimbabwe si mara ya kwanza kwani awali ilijulikana kama Rhodesia Kusini kati ya mwaka 1898-1964, ambalo ni la wakoloni wa Kiingereza.

Mwaka 1960, wazalendo walianza kuliita taifa hilo Zimbabwe. Jina hilo linalotokana na maneno mawili “dzimba” na “dzamabwe” yenye maana ya nyumba ya mawe kwa lugha ya Kishona inayozungumzwa maeneo mengi nchini humo, limekuwa utambulisho wa mafanikio ya nchi hiyo.

Nchi ya Burkina Faso ilipewa jina hilo na Rais Thomas Sankara akiibadili kutoka Upper Volta Agosti 1984.

Alilichagua jina hilo ambalo ni maneno mawili “Burkina” na “Faso” kutoka makabila mawili makuu yanayozungumzwa nchini.

Jina la zamani la Upper Volta lilitoka Ufaransa iliyokuwa ikiitawala nchi hiyo kutokana na mto wa Volta uliopita katika eneo hilo.

Burkina katika lugha ya Moore lina maana ya “wanaume wenye heshima” na Faso katika lugha ya Dioula lina maana “alikozaliwa baba” na yakichanganywa inakuwa Burkina Faso.

Tanganyika ndilo lililokuwa jina la Tanzania Bara ya sasa hadi mwaka 1964 liliporithiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Zanzibar ya zamani, kwa upande mwingine ilijumuisha visiwa vya Bahari ya Hindi vya Unguja na Pemba.

Ghana ilibadilisha jina lake kutoka Gold Coast mwaka 1957 kuendana na hadhi yake mpya ya kuwa jamhuri baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza.

Kiongozi wa kwanza wa Ghana, Dk Kwame Nkrumah alilipa Taifa hilo jina jipya muda mfupi baada ya kujinyakulia uhuru.

Kwa sasa Ghana inajivunia jina hilo lenye ishara ya mafanikio na uzalendo.

Nchi ya Swaziland ndilo Taifa la hivi karibuni kubadili jina ambalo Aprili, 2018 liliamua kujiita Jamhuri ya Ufalme wa eSwatini.

Jina hilo jipya lilitolewa na mfalme wa nchi hiyo, Mswati III katika sherehe za kuadhimisha miaka yake 50 na pia miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.

eSwatini yenye wakazi milioni 1.3 inapakana na Afrika Kusini na Msumbiji.