Mkutano wa Trump, Kim kufanyika Hoteli Capella

Muktasari:

  • Eneo la mkutano wa kilele kati ya Rais Trump na Kim Jong Un will litakuwa Hoteli Capella iliyoko kisiwa cha Sentosa.

Washington, Marekani. Mkutano wa kihistoria kati ya Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un uliopangwa Juni 12 utafanyika kwenye Hoteli Capella iliyoko katika kisiwa cha Sentosa Singapore, Ikulu ya White House imetangaza.
“Eneo la mkutano wa kilele kati ya Rais Trump na Kim Jong Un will litakuwa Hoteli Capella iliyoko kisiwa cha Sentosa. Tunawashukuru sana wenyeji wetu Singapore kwa ukarimu wao,” Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sarah Sanders alisema kupitia Twitter.
Kisiwa cha Sentosa kilikuwa kikiangaziwa kama moja ya maeneo yatakayotumika kwa ajili ya mkutano huo kutokana na eneo hilo kukidhi vigezo vya kiusalama.
Katika kuhakikisha usalama kuanzia Jumanne, Serikali ya Singapore ilikitenga kisiwa hicho na maeneo ya jirani kama eneo la tukio maalum na kuwa lipo chini ya ulinzi mkali.
Mkutano wa wakuu hao wa nchi utaanza saa 3:00 asubuhi kwa saa za Singapore sawa na saa 10:00 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki.

Programu ya nyuklia
Tayari Trump ameanza kupokea taarifa kuhusu programu ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini, ambayo itakuwa ajenda kuu, Ikulu imesema.
Trump mwenyewe alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisema, “Ninatumai mkutano na Korea Kaskazini nchini Singapore utakuwa mwanzo wa kitu kikubwa...tutaona hivi karibuni!"

Korea Kaskazini kujigharimia
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Heather Nauert amesema serikali haitalipia gharama za malazi za Korea Kaskazini katika mkutano wa viongozi wakuu wa nchi hizo mbili utakaofanyika wiki ijayo nchini Singapore.
Nauert alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne. Pia alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo aliishukuru serikali ya Singapore kwa ushirikiano kwa ajili ya mkutano huo unaotarajiwa kuandika historia mpya.