Mlipuko waripotiwa katika treni Uingereza

Muktasari:

  • Polisi wameuhusisha mlipuko huo na tukio la kigaidi.

London, Uingereza. Watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya kutokea mlipuko katika kituo cha treni ya chini ya ardhi kukiwa na msongamano wa watu Kusini Magharibi mwa London.

Katika tukio hilo ambalo polisi wanalihusisha na ugaidi, watu wa kutoa msaada wamesema waliitwa baada ya kupewa taarifa za moto kuzuka katika kituo cha treni cha Parsons Green saa 2:20 asubuhi.

“Ni mapema mno kuthibitisha kiini cha moto huo ambao unafanyiwa uchunguzi wa kina kwa sasa na kikosi cha kupambana na ugaidi,” taarifa ya polisi imesema.

Kamishana wa polisi Neil Basu, mratibu mwandamizi wa mapambano dhidi ya ugaidi ametoa taarifa inayoeleza kuwa tukio hilo ni la kigaidi.

Gazeti la Metro limeripoti kuwa, baadhi ya abiria wameungua usoni na wengine wameumia baada ya kukanyagana wakati wa kujiokoa.

Picha ambayo haijathibitishwa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha ndoo nyeupe ikiwa na begi maalumu kwenye sakafu ya behewa. Ndoo hiyo inaonekana ikiwaka moto na nyaya zikijitokeza juu.

Abiria katika kituo cha wazi cha Parsons Green kupitia mitandao ya kijamii wamesema baadhi ya watu wamepata majeraha usoni na kwamba, walikuwa na wasiwasi wakati watu walipojaribu kutoka ndani ya treni.

“Nilikuwa mtu wa pili kutoka kwenye behewa. Nilisikia mlipuko. Nilitazama na kuona behewa lote limegubikwa na miale ya moto na ukielekea kwangu,” alisema abiria Ola Fayankinnu aliyekuwemo kwenye treni.