Katumbi abeza amri ya kukamatwa kwake

Muktasari:

  • Waziri wa Sheria Alexis Thambwe Mwamba Alhamisi alisema hati imetolewa na kwamba serikali inataka akamatwe kokote atakakopatikana.

Windhoek, Namibia. Kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Moise Katumbi amesema serikali ilipaswa kumkamata alipokuwa anafanya juhudi za kutaka kurejea mapema mwezi huu.
Katumbi ametoa matamshi hayo siku moja tangu DRC itoe hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake tangu alipokimbilia uhamishoni mwaka 2016.
Waziri wa Sheria Alexis Thambwe Mwamba Alhamisi alisema hati imetolewa na kwamba serikali inataka akamatwe kokote atakakopatikana.
Lakini Katumbi akizungumza na shirika la BBC amehoji mantiki ya hati ya kukamatwa kwake.
“Wanawezaje kutoa hati ya kukamatwa kwangu wakati wiki mbili zilizopita walinizuia nilipotaka kurejea? Hivi sasa niko Namibia na wanaweza kunipata ikiwa wanataka kunikamata,” alisema.
“Maoni yangu ni kwamba madai hayo yanatolewa na ngoma tupu kama wanavyosema madebe matupu hayaachi kupiga kelele. Watu wanaowasababishia umaskini watu wa Congo ni wale walioko madarakani wanaotoa shutuma za uongo dhidi yangu.
“Ni wale wanaoiba na kuua watu hata sasa ndio wanapaswa kufikishwa kwenye mkono wa sheria.”
Katumbi alikuwa na matumaini ya kurejea DR Congo kabla ya Agosti 8 tarehe ya mwisho ya kujaza fomu za kuwania urais uliopangwa kufanyika Desemba.
Lakini kwanza alijaribu kusafiri kwa ndege hadi Lubumbashi akitokea Afrika Kusini lakini alizuiwa. Baadaye akatumia usafiri wa gari akitokea Zambia, lakini pia alizuiwa na mamlaka za DR Congo.