Aliyeua Marekani alikuwa na bunduki 42

Tuesday October 3 2017

 

Las Vegas, Marekani. Siku moja baada ya kutokea shambulio baya zaidi katika historia ya hivi karibuni nchini lililosababisha vifo vya watu 59 na majeruhi 527, polisi wamegundua mshambuliaji Stephen Paddock alikuwa na silaha 42 pamoja na vilipuzi.

Polisi walifanya ukaguzi wa kina nyumbani kwake karibu na Mesquite, Nevada, ambako walikuta bunduki 19, vilipuzi, maelfu ya risasi na vifaa vya kielektroniki.

Pia, katika chumba cha hoteli ya Mandalay Bay Resort and Casino ambamo Paddock alikuwa anaishi, polisi walikuta silaha 23, zikiwemo ‘handgun’ moja na ‘rifles’. Polisi walikuta ndani ya gari lake kilo kadhaa za ‘ammonium nitrate’ dawa inayotumika kutengenezea milipuko.

Madhumuni

Polisi wamepata ushahidi zaidi ambao wanaendelea kuunganisha ili kujua madhumuni ya shambulio hilo.

Hadi sasa hayajapatikana maelezo ya kutosha kwa nini Paddock, 64, mhasibu mstaafu ambaye hana rekodi yoyote ya uhalifu aliweza kuzua balaa kwa kuwamiminia risasi watu waliokwenda kupata burudani katika eneo la wazi la Jason Aldean lililokuwa limejaa watu 22,000 waliokuwa wakihudhuria tamasha.

Polisi wanaofanya uchunguzi kuhusu tukio hilo baya zaidi katika historia ya hivi karibuni nchini Marekani wanaamini alitekeleza shambulio hilo peke yake.

"Tunaamini Paddock alitekeleza peke yake shambulio hilo baya la mauaji," Mkuu wa Polisi Msaidizi Todd Fasulo aliwaambia waandishi wa habari.

Mkuu wa polisi wa Las Vegas, Joseph Lombardo aliwaambia waandishi wa habari kwamba Paddock alikuwa mzima alipokutana kwa mara ya kwanza na maofisa sita wa polisi katika hoteli hiyo waliofanya ukaguzi chumba kimoja hadi kingine usiku wa Jumapili.

Lombardo alisema Paddock aliwarushia risasi maofisa hao kupitia mlangoni na akampiga mguuni mlinzi wa usalama.

Maofisa wengine walipoingia kwenye chumba chake kwa kuvunja mlango walikuta Paddock akiwa amejiua kwa kujipiga risasi.

Kwa mwaka 2017 pekee asasi iitwayo Gun Violence Archieve imerekodi matukio 273 ya kushambulia watu. Asasi hiyo pia imerekodi vifo vya watu 11,621 wanaohusiana na matukio ya mashambuliao na wengine 23,433 waliojeruhiwa katika kipindi hicho.

Tukio la Mandalay Bay limekuja wiki chache tangu Spencer Hight alipofanya shambulio katika mkusanyiko nyumbani kwa mke aliyetengana naye huko Plano, Texas. Aliua watu wanane na yeye aliuawa na polisi.

 

 

 

 

Advertisement